Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mmoja wa wafanyakazi wa
Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL), wakati alipotembelea ofisi hizo
mkoani Mwanza.
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za
Meli Nchini (MSCL), Bw. Erick Hamis akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hali ya utendaji
wa kampuni hiyo katika ukanda wa Ziwa Viktoria, mkoani Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella,
akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa pamoja na menejimenti na wafanyakazi wa Kampuni ya Huduma
za Meli Nchini
(MSCL), wakati wa ziara ya Waziri huyo katika ofisi hizo
mkoani Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa amesema atabadilisha uongozi wa menejimenti ya
kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL), kwa kushindwa kutekeleza
uendeshaji na usimamizi wa kampuni hiyo.
Akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo
mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni
hiyo na kuonesha kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na MSCL, Prof.
Mbarawa amesema kutokana na kampuni kushindwa kujiendesha kibiashara na
kulipa mishahara kwa wafanyakazi wake amelazimika kuchukua maamuzi hayo
ili kuinusuru kampuni hiyo.
“Sijaridhishwa na taarifa za mahesabu yenu
katika uendeshaji wa huduma za meli katika ukanda wa Ziwa Viktoria,
Hamuwezi kusafirisha mizigo milioni 3.6 na nyie mkapata faida ya laki
2.. hamuomyeshi umakini kwenye utendaji”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha, katika kuhakikisha huduma za
Kampuni hiyo zinaimarika Serikali kupitia Waziri huyo imeahidi kutoa
kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukabarati wa meli nne
zilizokuwa zimekufa katika ukanda huo ili kuboresha huduma za usafiri wa
Ziwa.
Prof. Mbarawa amezitaja meli
zitakazokarabatiwa ni Mv. Clarious, Mv Serengeti, Mv Sangara na Mv.
Ukerewe ambazo zinahitaji ukarabati wa injini, mifumo ya umeme na ufundi
na gia boksi.
Amewatahadharisha watumishi wachache
wanaofuja fedha katika kampuni hiyo na wale wazembe wanaoshindwa
kutekeleza majukumu yao kuacha maramoja kwani Serikali haitamvumilia
mtumishi anayefanya vitendo hivyo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa
Kampuni hiyo, Bw. Erick Hamis, amezitaja changamoto mbalimbali
zinazoikabili MSCL, kuwa ni uhaba wa watumishi wenye weledi na ujuzi
hususan wenye taaluma ya uhandisi na kukosekana kwa mfumo imara na
wakisasa wa udhibiti na ukusanyaji mapato.
“Kampuni inapoteza mapato kutokana na
mfumo wa kizamani wa ukusanyaji mapato, fedha nyingi zimekuwa zikipotea
na kutumika kusikojulikana, hivyo basi tumeamua kuhakikisha tunaboresha
mfumo huu ili kupata mapato zaidi”, amesema Kaimu Meneja Mkuu.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John
Mongella, ameipongeza serikali kwa hatua iliyochukua ya ukarabati wa
meli ya Mv Serengeti ambayo ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Bukoba katika
usafirishaji wa ndizi na mbao.
Amewasihi wafanyakazi kuondoa dhana
iliyojengeka ya kufanya kazi kiholela na kwa mazoea na badala kutoa
ushirikiano kwa Kaimu Mkuu huyo na Menejimenti itakayoundwa ili kufufua
upya kampuni hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Post A Comment: