Nianze kwa kumshukuru Mungu wa Mbinguni kwa kunijalia afya njema na uwezo wa
kufanya kazi kwa bidii na maarifa, namshukuru kwa neema na baraka zake katika maisha yangu ya
kila siku na familia yangu, pia namshukuru Mke wangu kipenzi Deborah Maduka na Mwanangu Isaac Joel wazazi wangu pamoja na wazazi wa mke wangu hawa ni watu ambao kila siku wananipa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii na kutafuta mafanikio sijajuta kuwa na familia hii ambayo Mungu amenipatia namshukuru kwa wewe msomaji wa mtandao huu ambae umeendelea kunifatilia kila siku kupitia masomo mbali mbali na mwisho Namshukuru sana Mungu kwa muongozo anaonipa katika kuishi na watu
wanaonizunguka.
Nampenda kama anavyonipenda na ninamshukuru kwa kunipa nafasi nyingine
kila siku niweze kufikiria toba ya kweli ili nitakapolala nipumzike
katika amani ya milele nikiwa upande wa mkono wake wa kuume.
Katika maisha, hakuna kitu kinachoweza kufanyika kama hakutakuwa na bidii ya utendaji.
Huo ndiyo ukweli, bidii ni kiungo muhimu sana katika kufanikisha jambo lolote kwa mtazamo chanya.
Lakini bidii peke yake inatosha kukamilisha mafanikio maishani? Jibu ni
kwamba si kweli kwani pamoja na bidii kuwa kiungo muhimu cha mafanikio,
lakini bado kuna vitu vingine muhimu zaidi ili kujipatia maendeleo na
mafanikio maishani ambavyo ni Uaminifu, Ukweli na Imani.
Vitu hivi kwa pamoja vinakamilisha nguzo kuu muhimu maishani kwa mtu
aliyedhamiria kupata mabadiliko. Katika kila jambo unalofanya, hakikisha
kuwa unalifanya kwa bidii huku akili na nguvu zako zikiwa kwa asilimia
95, ukifanya hivyo lazima utapata mafanikio.
Baada ya kuwa na bidii kwa kiwango hicho, jambo linalofuata ni uaminifu
wako katika mazingira unayofanyia kazi. Kumbuka kuwa uaminifu haujali
kama wewe ni mfanyakazi au mfanyabiashara bali kwa kila eneo unalofanyia
kazi hakikisha kuwa unakuwa muaminifu kwa kiwango kikubwa. Uaminifu
katika kazi zako lakini pia uaminifu kwenye mali za wengine.
Mathalani bosi wako amekuagiza kufanya jambo linalohitaji fedha nyingi,
basi usifanye ujanja wowote kuzidisha kiwango cha kawaida kwani kufanya
hivyo si ujanja badala yake ni kujiwekea mazingira magumu sana maishani.
Hivyo uanimifu ni nguzo nyingine muhimu sana katika safari ya kutafuta mafanikio maishani mwako.
Unapokopa fedha au kitu flani kwa mtu, hakikisha unakirejesha kwa muda
mliokubaliana, achana na tabia ya kudhulumu vitu ambavyo si halali kwako
kwani utafiti wa kisaikolojia unaonesha kuwa, mali zote zinazopatikana
kwa njia za mkato au njia ambazo si za uaminifu mara nyingi huwa
hazidumu.
Hivyo msomaji wangu, jitahidi sana kuboresha eneo la uaminifu katika mazingira unayojipatia riziki maishani mwako.
Lakini pia, nguzo nyingine ni Ukweli kwani ukitaka kuishi maisha ya
amani na yenye furaha basi jitahidi sana kusema ukweli kwa kila sentensi
inayotoka kinywani mwako. Katika ofisi ninayofanyia kazi, ninashika
nafasi ndogo sana ya uongozi lakini kitu ambacho huwa nasisitiza kwa
wafanyakazi wenzangu ni kusema ukweli.
Achana na ahadi ambazo unajua kabisa kwamba huwezi kuzitimiza kwani
ukijijengea mazingiara ya uongo katika jamii unayoishi basi utakuwa
unafukuza myanya ya mafanikio maana unaweza kuwa na kitu cha muhimu sana
kukifanya lakini kwa kuwa umejijengea mazingira ya uongo basi hakuna
atakaye kuamini.
Ukiwa msemakweli, hautalaumiwa na mtu na wala hutamlaumu mtu.
Mfano, rafiki yako anakuomba umfanyie jambo flani kwa wakati maalum na
wewe unakubali japo unakuwa na uwezo mdogo kufanya hivyo, unafikiri kama
muda ukifika na haujafanya kitu hicho ni nini kitafuata? Jibu ni
lawama kwani umeahidi kitu ambacho huwezi kukifanya na siku nyingine
hawezi kukuamini.
Juu ya hayo yote kuna kitu muhimu zaidi ambacho ni Imani.
Hapa ndipo kwenye kiini kikubwa cha mafanikio maishani kwani hata kama
unafanya kazi kwa bidii kiasi gani, ni mkweli kwa kiasi gani lakini kama
hauna imani na unachokitaka basi ni vigumu kufanikiwa.
Yaani kama wewe unataka kuwa mwanasheria lakini huna imani na ndoto yako, basi elewa ni vigumu mno kufanikiwa katika hilo.
|
Post A Comment: