Na
Ismail Ngayonga
Serikali imesema ipo mbioni kuanzisha mfumo wa utambuzi na usajili wa barabara zote
nchini, hatua inayolenga kuziwezesha barabara zote kujengwa katika viwango
vinavyofafana na ubora wa huduma ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa
wananchi hususani wa maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa leo
Wilayani Handeni Mkoani Tanga na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Elias Kwandikwa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi
wa barabara katika Wilaya za Handeni, Kilindi na Korogwe.
Kwandikwa alisema ili
kutekeleza adhma hiyo, Serikali imekusudia kuiwezesha Wakala wa Barabara za
Mijini na Vijijini (TARURA) kwa kuiongezea uwezo wa vitendea kazi na waatalamu
wa kutosha ili kuhakikisha kuwa miradi ya barabara iliyopo katika Halmashauri
zote nchini inakuwa na chombo maalum cha usimamizi.
“Ni wajibu wa
Watendaji wote kushirikiana katika kusimamia miradi ya barabara, kwa kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa TARURA ikiwemo kuipata fedha pale inapokwama katika kutekeleza
wajibu wake hususani katika maeneo korofi yanayohitaji fedha maalum” alisema
Kwandikwa.
Alisema kukamilika
kwa miradi ya barabara katika maeneo mengi ya vijijini kutawezesha wananchi
kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uzalishaji
na usafirishaji wa mazao na pembejeo na hivyo kuvutia uwekezaji katika miradi
mikubwa ya maendeleo.
Aidha Kwandikwa
alisema ili kutekeleza vyema majukumu yake, ni wajibu pia wa TARURA kujisogeza
karibu zaidi kwa jamii ikiwemo kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi na
Viongozi mbalimbali katika Mamlaka ya Serikali za mitaa, hatua inayolenga
kujenga uelewa wa mamlaka, wajibu na majukumu ya taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa
asilimia 80 ya uwezeshaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini unategemea
upatikanaji wa miundombinu ya barabara za uhakika, hivyo ni wajibu wa TARURA
kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kuinua
uchumi pasipo kukabiliwa na changamoto zisizo na ulazima.
Akifafanua zaidi
Kwandikwa alisema Serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushirikiano
unaohitajika ikiwemo kupokea ushauri, mapendekezo na maoni kuhusu hatua
mbalimbali zinazopaswa katika kuboresha na kusimamia miundombinu ya barabara inayosimamiwa
na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema Wilaya yake imejipanga kikamilifu
katika kuhakikisha kuwa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinafuatwa katika
usimamizi wa miundombinu ya barabara kwa kuwa hatua itasaidia kuleta maendeleo
ya haraka kwa wananchi.
“Wilaya imejipanga
kikamilifu katika kusimamia sheria ikiwemo kudhibiti mifugo inayovuka kutoka
upande mmoja wa barabara kwenda mwingine, kwa kuwa mara nyingi imekuwa
ikichangia uharibifu wa miundombinu ya barabara zetu” alisema Gondwe.
Post A Comment: