Mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana katika eneo la mtaa wa Miti mirefu wilaya na mkoa wa Geita.
Tukio hilo limetokea majira ya usiku wa kuamkia leo ambapo marehemu aliyefahamika kwa jina la Lucas Dagadaga 65 mkazi wa kijiji cha Mbabane, ambaye alikuwa ni mlinzi wa maduka ya mtaa huo, ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani akiwa katika eneo la lindo lake.
Storm habari imefika katika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi ya mashuhuda ambapo wamesema kuwa suala la mauaji mkoani hapa limekuwa likijitokeza mara kwa mara huku wakililalamikia jeshi la polisi kushindwa kuchukua hatua dhidi ya matukio yanayokuwa yakijitokeza kwani tukio la kuuawa kwa walizi sio la kwanza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kuwa baada ya mauaji hayo watuhumiwa walivunja duka la Adinani Dauda 36 mfanyabiashara wa eneo hilo na kupora fedha kiasi cha shilingi 800,000, vocha mbalimbali zenye thamani ya tsh 100,000 sambamba na simu 7 za wateja zilizokuwa zikichajiwa dukani hapo ambapo wamiliki na thamani yake bado hazijaweza kufahamika.
Aidha kamanda Mponjoli ametoa wito kwa waajiri kuacha tabia ya kupenda vitu rahisi kwa kuajiri walinzi wasiokuwa na viwango na badala yake kuhakikisha wanaajiri watu walio na viwango vya ulinzi ili kuepusha maujai hayo.
Post A Comment: