WIMBO WA RAIS MAGUFULI KUZINDULIWA WIKI HII.

Share it:








Rais John Magufuli akionesha usitadi wake wa kupiga Ngoma.





MWANAMUZIKI nguli mwenye makao yake jijini Nairobi nchini Kenya, Skassy Kasambula amekamilisha wimbo maalumu wa kusifu kazi za rais wa Tanzania wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli. 

Kasambula alisema kuwa si yeye tu, bali wananchi wengi nchini Kenya wanamkubali Rais Magufuli na kwamba anashangaa hadi sasa hakuna nyimbo za kutosha kutoka kwa wasanii wa Tanzania, kwa ajili ya kumpongeza kiongozi huyo kwa juhudi zake za kuleta usawa baina ya masikini na matajiri. 

Wimbo ‘Heko Rais Dokta Magufuli,’ umeimbwa na Skassy akishirikiana na bendi yake mpya ya Orchestra Safari Star ya jijini Nairobi, kundi ambalo pia hivi karibuni lilitoa wimbo kumsifu rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta pamoja na makamu wake William Ruto. 

Akizungumza kwa njia ya mtandao, Kasambula alisema wimbo wa Magufuli hautakuwa kwenye albamu yake mpya yenye nyimbo 10 bali utabaki kuwa ‘single,’ na kwamba utaanza kusikika nchini wiki hii mara baada ya kuwapata wasambazaji, na kwamba baadhi ya vituo vya radio vitatumiwa nakala. 

Kasambula sio mgeni Tanzania, aliwahi kuishi nchini akiimba katika bendi kadhaa katika miaka ya 1980 na 1990, ikiwemo Super Matimila ambayo ndio hasa ilimleta nchini kutoka Zaire (DR Congo), Orchestra Tomatoma, Orchestra Safari Sound, Sambulumaa Band na Ngorongoro Heroes. 

Baadhi ya kazi zake maarufu akiwa nchini ni pamoja na wimbo ‘Christina Moshi’ akiwa na Safari Sound, ‘Mayombo,’ akiwa na Sambulumaa, pamoja na kibao cha ‘Bishada,’ akiwa na Super Matimila. 

Na katika albamu yake mpya itakayotoka hivi karibuni mwanamuziki huyo gwiji, ambaye siku hizi anajulikana kama ‘Sultani Skassy Kasambula,’ pia amezirudia baadhi ya nyimbo zilizowahi kuwika nchini ukiwemo ‘Marashi ya Pemba,’ wa Ndala Kasheba na wimbo wake mwenyewe ‘Christina Moshi.’ 

Wakati huo huo, msanii wa bongo fleva Nice Lucas Mkenda maarufu kama ‘Mr Nice,’ aliyewahi kutamba na wimbo ‘Fagilia,’ miaka 13 iliyopita, ametangaza kurudi tena kwenye fani akitarajia kufyatua albamu yake mpya itakayojulikana kama ‘Kioo!” Mr Nice, hata hivyo ameamua kwenda kuizindua albamu hiyo jijini Nairobi nchini Kenya ambako ndiko hasa alikofanya mahojiano rasmi kuhusu ujio wake mpya, kwenye kituo cha Televisheni cha ‘Citizen Tv.’ 

Mkazi huyo wa Sinza Dar es Salaam, alidai kuwa ana mashabiki wengi nchini humo kuliko hata Tanzania, na kwamba ataanza na maonesho kadhaa nchini Kenya. Imeandikwa na Marc Nkwame, 

Arusha/Habarileo

Share it:

habari

Post A Comment: