LICHA ya takwimu za hivi karibuni kuonesha uchumi wa Taifa pamoja na
Pato la Taifa vimekuwa vikikua kwa kasi na kuifanya Tanzania kuwa moja
ya nchi zenye uchumi imara, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imedai kuwa
uchumi wa Tanzania umeyumba.
Kambi hiyo imetaja baadhi ya maeneo yanayothibitisha hilo kuwa ni mikopo
inayotolewa na benki za biashara kwenye sekta binafsi kuwa imeshuka
katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Halima Mdee alisema mikopo
hiyo imefikia Sh bilioni 1,167.2 ikilinganishwa na ongezeko la Sh
bilioni 1,577.5 la mwaka 2015 katika kipindi kama hicho.
“Hii maana yake sekta binafsi imekosa Sh bilioni 410.3 katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2016. Hali hii imefanya mzunguko wa sarafu na noti
mikononi mwa watu kushuka kutoka asilimia 188.8 Desemba 2015 na kufikia
asilimia 6.7 Julai mwaka 2016,” alieleza.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amana za
wateja katika benki zilipungua kutoka Sh trilioni 20.52 Desemba 2015
hadi kufikia Sh trilioni 20.24 Juni mwaka 2016.
Akichangia mapendekezo ya mpango huo wa maendeleo, Mbunge wa Sikonge,
Joseph Kakunda (CCM) alisema takwimu zinaonesha asilimia 53 ya viwanda
vikubwa nchini vipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Kagera na Arusha,
uwiano ambao si mzuri na kutaka viwanda viwepo kwenye mikoa mingine pia.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa
Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Dk Albina Chuwa, katika kipindi cha
robo ya pili ya mwaka huu, Pato la Taifa limeendelea kukua kwa kasi ya
asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 5.8 ya robo ya pili ya mwaka
jana.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu alisema
ukuaji wa Pato la Taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka ya Januari hadi
Juni, umeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.7 kwa nusu
ya kwanza ya mwaka 2015.
Navigation
Post A Comment: