WACHANJWA CHALE KUONGEZEWA UJASIRI

Share it:




WAKATI majeshi mengine yakijiimarisha kijasiri na ukakamavu kwa kufanya mazoezi ya mwili kwa vifaa bora, askari wa jadi, maarufu sungusungu ambao ni vijana wa kiume wapatao kiume 83 wamelazimika kuchanjwa chale mwili mzima kuongezewa ujasiri.

Vijana hao walichanjwa chale na waganga wa kienyeji ili wawe wakali pia wawe jasiri wanapokabiliana na wahalifu hata kama wahalifu wana silaha nzito.

Sherehe ya kuchanjwa ilihusisha sungusungu wa vijiji vya Mwale na Ng’ongo vilivyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa katika wilaya ya Sumbawanga, Rukwa, ambako mbuzi wawili walichinjwa kwa ajili ya kitoweo cha askari hao. Walikula kwa ugali wa dona.

Gazeti hili lilifika uwanja uliotumika kwa sherehe hizo ndani ya msitu huo na kushuhudia askari hao vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 40 wakichanjwa chale mwili mzima na waganga wanne wa kienyeji waliokodishwa kuifanya kazi hiyo .

Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini, vijana wengine wa miraba minne walidai kuwa na imani ya dawa hizo za kienyeji kuwa zina uwezo wa kuwafanya kuwa wakali na jasiri zaidi.

“Tukishapigwa chale mwili mzima basi tutakuwa na uwezo wa kubaini mhalifu kabla hata hajafanya uhalifu hivyo tutaweza kuzuia uhalifu kabla haujafanyika. Isitoshe tutakuwa jasiri kupita kiasi, nguvu za kupita kiasi na hatutaogopa kukabiliana na mwalifu hata kama atakuwa na silaha nzito,” alisisitiza mmoja wao .

Akizungumza na gazeti hili Kamanda wa Jeshi hilo la Sungusungu, Mahona Boniface alisema kupigwa chale kwa askari hao vijana wa sungusungu ni agizo la mtemi wao wa sungusungu aitwae Clement Mbogatabu alilolitoa mara baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.

“Mie ndiye niliyepiga mbiu kuwakusanya askari hawa na kuwapatia maagizo ya mtemi wetu wa sungusungu wote waliafiki na leo (juzi) tumekusanyika kwenye uwanja huu ambapo kila askari ameagizwa aje na wembe wake mwenyewe mpya na kiasi cha Sh 500 ikiwa ni ujira wa mganga atakaye mchanja chale,” alisema Mbogatabu.

Waganga hao wa kienyeji waliokodiwa kuifanya kazi hiyo walitajwa kuwa ni Juma Aron, Shinje Buzuka na Lutema Mugesa huku jina la mganga wa nne halikuweza kupatikana.

Alisema waganga hao wanatoka kijiji cha Uzia na mwingine ni mkazi wa kijiji cha Santaukiwa vilivyopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ambapo shughuli hiyo walifanya juzi kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana .

Walisema baada ya kuchanjwa askari hao vijana wa kiume wa sungusungu wamezuiwa kukutana kimwili na mwanamke hata kama wameoa kwa muda wa siku tatu baada a kupita siku hizo watakusanyika tena ambapo wataogeshwa dawa ndipo wataruhusiwa kufanya tendo la ndoa.
Share it:

matukio

Post A Comment: