Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo akielezea
utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu inayosimamiwa na Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) kwenye kituo cha redio cha TBC
Na
Greyson Mwase, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt.
Mhandisi Juliana Pallangyo amesema kuwa Bandari ya Tanga inatarajia kuwa ya kimataifa kabla na baada ya kukamilika kwa Mradi wa
Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika
Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Dkt. Pallangyo
aliyasema hayo tarehe 03 Agosti, 2017 jijijni
Dar es Salaam kupitia mahojiano maalum
kwenye kipindi cha Jambo
Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kupitia
kituo chake cha TBC1 lengo likiwa ni kuelezea uzinduzi wa Mradi wa Bomba hilo
utakaofanyika Agosti 05, 2017.
Alisema kiasi
cha Dola za Marekani milioni 200
kinatarajiwa kupatikana kama kodi wakati wa ujenzi na kuongeza kuwa mradi
utatoa takribani ajira 10,000 kwa watanzania
hususan katika maeneo yatakayopitiwa na miundombinu ya Bomba hilo.
Alisema Serikali
kupitia Wizara ya Nishati na
Madini imejipanga katika kuhakikisha
kila mwananchi aliye karibu na
miundombinu ya Bomba hilo anakuwa sehemu ya uchumi wa bomba husika kupitia ajira na utoaji wa huduma mbalimbali.
Aidha, alitoa rai kwa wananchi husuan waliopo katika maeneo
yatakayopitiwa na bomba hilo kujinga na Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na
Gesi Tanzania (ATOGS) itakayokuwa na
jukumu la kuwaunganisha watoa huduma wote na kuwapa elimu ya namna bora
ya kupata mikopo katika taasisi za
serikali na kutoa huduma bora kwa kampuni zitakazojenga bomba hilo.
Akielezea usalama wa bomba hilo, Dkt. Pallangyo
alisema Serikali imepanga mkakati maalum wa utoaji elimu kwa wananchi waishio
karibu na miundombinu ya Bomba ili wawe walinzi na kufunga mfumo maalum wa
usalama kwenye Bomba.
Katika hatua nyingine, akielezea maandalizi ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa Gesi na Mafuta, Dkt. Pallangyo
alisema Serikali kupitia Wizara ya
Nishati na Madini imekuwa ikitoa ufadhili kwa wataalam wake na wanafunzi wanaofanya
vizuri katika masomo ya Sayansi kwenda kusoma nje ya nchi masuala ya Mafuta na
Gesi.
Aliongeza kuwa, kozi kuhusu masuala ya Mafuta na Gesi imekuwa ikitolewa
katika vyuo vikuu kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Akielezea utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu inayotekelezwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.
Pallangyo alisema utekelezaji utahusisha vipengele vitatu ambavyo ni pamoja na kusambaza umeme katika maeneo ambayo
hayajafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme na kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika
vijiji ambavyo vimefikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya
maeneo na vitongoji havikuungwa.
Aliendelea kueleza kuwa
Kipengele cha Tatu kinahusisha usambazaji wa umeme utokanao na vyanzo vya Nishati Jadidifu
kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi hususan
visiwani.
Alisisitiza kuwa
lengo la REA Awamu ya Tatu ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinafikiwa
na umeme ifikapo mwaka 2021
Wakati huo huo, akielezea mradi wa kuzalisha umeme
kwa kutumia maji wa Stiegler’s Gorge wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2100,
Dkt Pallangyo alisema kuwa maandalizi yameshaanza kwa timu ya wataalam kupitia tafiti mbalimbali
zilizowahi kufanywa kuhusu mradi huo na
kubadilishana uzoefu na wataalam kutoka nchi ya Ethiopia ambao ni wazoefu kwenye ujenzi wa mabwawa na mitambo ya
kuzalisha umeme kwa njia ya maji.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutapelekea nchi
kupata Umeme wa uhakika na kuchochea kuongezeka kwa uwekezaji kwenye uchumi wa
Viwanda.
|
Post A Comment: