Mmoja wa
wazazi wa wanafunzi walioondolewa shuleni kutokana na kukosa sifa za kusoma
katika shule za Sekondari za Serikali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa na
viongozi wengine wa Serikali katika kikao kilichofanyika Shule ya Sekondari
Nkoma wilayani Itilima kujadili suala hilo.
Na
Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi
wa Halmashauri Mkoani humo kuunda timu zitakazopitia na kujiridhisha juu ya majina ya wanafunzi 633 waliotajwa kuwa
Mamluki na kuondolewa shuleni kwa kukosa sifa za kusoma shule za sekondari za
Serikali kutokana na sababu mbalimbali.
Agizo hilo amelitoa katika Shule ya Sekondari Nkoma wilayani
ITILIMA kwenye kikao chake na viongozi,
watendaji wa Serikali na wazazi wa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walioondolewa
katika mfumo wa Serikali kutokana
na kutumia majina yasiyo yao, kukosa fomu za TSM 9 , kukosa vibali vya kukariri/kurudia
kidato na vibali vya uhamisho.
Mtaka
amesema timu hizo zitakazoundwa kwa kila Wilaya zifuatilie na kujiridhisha kwa
kupitia majina yote pamoja na sababu za
wanafunzi hao kuitwa Mamluki na kuondolewa katika mfumo wa Serikali zilizoanishwa,
ambapo amebainisha kuwa watendaji wa Idara ya Elimu watakaobainika kusababisha
kwa uzembe wanafunzi hao kuondolewa shuleni watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ameongeza
kuwa Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa
Elimu Sekondari waitishe vikao na wanafunzi hao na wazazi wao, ili wazungumze
na kuwaeleza hatua zitakazochukuliwa baada ya kujiridhisha, baadaye taarifa ya
kila wilaya iwasilishwe mkoani.
“Kufikia
Ijumaa wakuu wote wa Wilaya na Maafisa Elimu wawe wamekutana na wanafunzi
waliopata matatizo hayo,wazazi wao na watoto wote waitwe kutoa ushuhuda wa nini
kimesababisha wao kuitwa mamluki na kurudishwa nyumbani, wakishajiridhisha watuletee hiyo taarifa na
sisi Mkoa tutaipitia na kutoa maelekezo; tunaweza kusema wanafunzi 633 ni mamluki
kumbe umamluki wa baadhi ya wanafunzi umesababishwa na uzembe wa Watendaji wetu.” alisisitiza Mtaka.
Aidha
baada ya kusikiliza hoja za baadhi ya wanafunzi walioondolewa katika mfumo wa shule
za Serikali pamoja na wazazi wao shuleni
Nkoma na kubaini kuwa baadhi ya sababu zilizopelekea wanafunzi hao kuondolewa
zimechangiwa na uzembe wa baadhi ya Watendaji wa Idara ya Elimu ngazi ya Wilaya
na Wakuu wa Shule Mtaka ameagiza wanafunzi hao warudishwe shuleni mara moja.
“Kuna
wanafunzi hapa Nkoma tumewasikiliza kesi zao wapo ambao walipaswa kurudia
darasa , taratibu za upatikanaji wa kibali cha kurudia darasa kama wanafunzi
pamoja na wazazi wamefanya, lakini inaonekana kuna uzembe kati ya Wakuu wa
Shule na Idara ya Elimu Wilaya, maagizo ya Serikali ya Mkoa vibali vya
wanafunzi hao kufikia tarehe 29/11/2017 viwe vimetolewa na warudishwe shuleni”
amesema Mtaka.
Sanjari
na hilo Mtaka ameagiza wanafunzi wote wanaosoma shule za Sekondari kwa kutumia majina
ya watu wengine waondolewe katika mfumo wa shule za Sekondari za Serikali na
akatoa wito kwa wazazi wao kuwapeleka katika shule binafsi au katika utaratibu
wa utahiniwa binafsi (QT) ili wafanye mitihani kama watahiniwa binafsi (Private
Candidates).
Baadhi
ya wanafunzi waliondolewa katika mfumo wa Shule za Serikali katika Shule ya
Sekondari Nkoma Wilayani Itilima kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutumia
majina ya watu wengine wamesema wako tayari kuendelea na masomo ikiwa watapata
nafasi katika shule binafsi, ambapo wazazi wao pia wamesema wako tayari kuwapeleka
watoto wao katika shule binafsi ili kuwasaidia wafikie malengo yao.
“ Nilipata
taarifa kuwa mwanangu ameondolewa shuleni kwa sababu anatumia jina la mtu
mwingine na nimeshaanza kutafuta nafasi kwenye shule za binafsi ili aendelee na
masomo kwa sababu alikuwa anafanya vizuri darasani, kwa mfano muhula uliopita
aliongoza” alisema Sumuni Daudi mmoja wa wazazi walioshiriki kikao na Mkuu wa
Mkoa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga
ameomba kuwepo na darasa maalum kwa wanafunzi watakaobainika kuwa siyo halali waandaliwe
utaratibu wa kufundishwa na baadaye wafanye mitihani kama
watahiniwa wa kujitegemea ili waweze kutimiza ndoto zao.
|
Post A Comment: