Na Stella
Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.Joseph Kakunda
ameiagiza mikoa na Halmashauri zote Nchini kuhakikisha kuwa zinaunda Kamati za
kushughulikia mahitaji ya watu wenye Ulemavu katika kila Halmashauri, Kata na
Vijiji, kabla ya June 30, 2018.
Mhe. Kakunda ametoa agizo hilo wakati wa Maadhimisho
ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani, ambayo yameadhimishwa Kitaifa katika
Uwanja wa Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu.
Amesema Serikali imetenga shilingi milioni 50
kuliwezesha Baraza la wenye Ulemavu Kitaifa kufanya kazi zake kwa mujibu wa
Sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Kamati zinaundwa hadi ngazi ya vijiji,
ili kufanikisha azma hiyo, amesema
lazima ziundwe kamati za kushughulikia wenye ulemavu katika kila Halmashauri,
Kata na Vijiji, ambapo ameipongeza mikoa ya Simiyu,, Tabora na Mbeya kwa
kukamilisha zoezi hili.
“Naipongeza mikoa ya Simiyu, Tabora na Mbeya kwa
kuanzisha kamati hizo katika Halmashauri zao
zote, naagiza Kamati hizo ziundwe katika mikoa yote na katika
Halmashauri zote nchini, wale ambao bado hawajakamilisha wakamilishe; tunataka
kuona ifikapo tarehe 30 Juni 2018 mikoa yote iwe na kamati hizo” amesisitiza
Kakunda.
Mhe.Kakunda pia ameziagiza Halmashauri zote Nchini
kuwapa Kipaumbele Wajasiriamali wenye Ulemavu katika utoaji wa Mikopo
inayotokana na asilimia 10 ya Mapato ya ndani ili waweze kujipatia mitaji ya
kuendeshea shughuli zao mbalimbali za ujasiriamali na kujikwamua kiuchumi.
Ameongeza kuwa Serikali imeandaa utaratibu wa Bima
ya Afya kwa watu wote wakiwemo wenye ulemavu ambao ujumuisha upatikanaji wa
huduma tengamavu na vifaa saidizi na itaendelea kuagiza na kutoa vifaa hivyo kwa
watu wenye ulemavu.
Aidha, amesema Serikali itahakikisha miundombinu
inakuwa rafiki na fikivu kwa wenye ulemavu, itaangalia namna bora ya
upatikanaji wa ajira kwao, itawahimiza
wamiliki wa vyombo vya habari kutumia wakalimani wa lugha ya alama, kuendelea kuchukua
hatua kadi dhidi ya wanaofanya ukatili kwa wenye ualbino, italifanyia kazi
suala la ukosefu wa Ofisi kwa ajili ya SHIVYAWATA kwa kuangalia uwezekano wa
kushirikisha Halmashauri kutenga Ofisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Bi.Ummy
Nderininanga akiwasilisha risala ya watu wenye Ulemavu, ametoa mapendekezo
kadhaa kwa Serikali na kuomba yafanyiwe kazi ikiwa ni pamoja na watu wenye
ulemavu kupatiwa bima za afya,upatikanaji wa ofisi za SHIVYAWATA, kuongezwa kwa nafasi za ajira kwa watu wenye
ulemavu, kutoa mikopo kwa watu wenye ulemavu,kuongeza ulinzi kwa watu wenye
ualbino na wanafunzi wa elimu ya juu wenye ulemavu kupewa ruzuku badala ya
mikopo, ambayo yote yalitolewa ufafanuzi na Viongozi wa Serikali.
Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anyeshughulikia wenye Ulemavu, Mhe.Stella Ikupa amesema Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza
kutoa kipaumbele na kujumuisha
watu wenye ulemavu katika mpango wa ukuzaji ujuzi unaoendeshwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu na pia imeanza kujadili kuona ni jinsi gani mikopo ya elimu
ya Juu itatolewa kama ruzuku kwa watu wenye ulemavu.
Akiwasilisha salamu za Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu Mkuu wa Wilaya ya Bariadi
Mhe.Festo Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu umeweka utaratibu maalum wa kuwatambua
watu wenye ulemavu kuanzia ngazi za vijiji na kubainisha kuwa hadi kufikia
mwaka 2017 jumla ya watu 6305 wenye ulemavu mbalimbali wametambuliwa.
Maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu mwaka 2017
yamebeba Kauli Mbiu isemayo , yenye Kauli Mbiu isemayo “BADILIKA TUNAPOELEKEA JAMII
ENDELEVU NA IMARA KWA WOTE” na
ni mara ya kwanza kufanyika Mkoani Simiyu.
Post A Comment: