Wakulima wa Pamba wakipanda mbegu za pamba katika kijiji cha Ng'hoboko wilayani Meatu mkoani Simiyu kwa kutumia mashine ya kupandia (seed Planter) inayokokotwa na wanyama. |
Robert Ngoko Mkulima wa Pamba, akipanda mbegu kwa kutumia mashine ya kupandia (seed Planter) aliyowezeshwa na kampuni ya bioRe Tanzania. |
NA COSTANTINE MATHIAS, MEATU.
WAKULIMA wa Pamba Wilayani Meatu mkoani Simiyu wameiomba serikali kuwapatia zana za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuweza kufikia na uchumi wa kati pia kujikwamua kimaisha.
Robert Ngoko ambaye ni mkulima wa Pamba alisema kuwa vitendea kazi vinasaidia kurahisisha kazi na kumaliza kupanda na kupalilia shamba kwa wakati, na kuitaka serikali kuwasogezea zana hizo ambazo wanaweza kujinunulia wenyewe.
Ngoko aliongeza kuwa kwa sasa anatumia zana za kilimo za kupandia (planter) ili kurahisisha kazi lakini zana hizo ni chache na wamewezeshwa na kampuni ya bioRe Tanzania inayojishughulisha na kilimo cha Pamba hai.
Naye Bulugu Sitta alisema kuwa alianza kilimo cha Pamba kwa miaka mitatu sasa na ameshaona mabadliko baada ya kuanza kilimo cha kisasa kwa kufuata ushauri wa wataalamu.
Alisema kuwa wamekuwa wakitembelewa na kushauriawa na mabwanashamba wa bioRe, juu ya matumizi ya zana za kilimo lakini changamoto kubwa ni uhaba wa zana za kilimo hali inayowafanya kusuburiana wakati wa upandaji na upaliliaji.
Hosea Magumba mkulima wa pamba kutoka Ng’hoboko alisema kuwa utaratibu wa mashamba darasa umesaidia kuwaimarisha wakulima kwa sababu wamekuwa wakitembelewa mara kwa mara na kupatiwa misingi ya kilimo cha pamba.
Kwa upande wake Charles Mabuga ambaye ni Mwezeshaji Wakulima toka kampuni ya bioRe Tanzania alisema kuwa wanawawezesha wakulima katika kilimo cha pamba na wamweza kuwapatia vipandio vya pamba (seed planter).
Alisema kuwa walianza kuwafundisha wakulima kupitia mashamba darasa juu ya teknolojia ya upandaji na upaliliaji, wawesamba mashine 50 kwa wakulima lakini uhitaji wa zana hizo umekuwa mkubwa baada ya wakulima kupata mwamko namna zinavyorahisisha kazi.
Aliongeza kuwa wakulima wanahitaji sana zana hizo, lakini upatikanaji wake ni mdogo huku mahitaji ni mkubwa na kuitaka serikali kuwasogezea zana hizo ili waweze kuzipata kwa ukaribu kwa sababu zinatengenezwa na shirika la kiserikali la CAMATEK lililoko Arusha.
Mkurugenzi wa Kampuni ya bioRe Tanzania inayojishughulisha na kilimo cha Pamba hai (organic cotton) Niranjan Pattni, alisema kuwa kwa sasa wameongeza wakulima wa pamba na kufikia 2045.
Alisema kuwa wakulima hao wamegawiwa mashine za kupandia bure ili kurahisisha upandaji ambapo wilaya ya meatu imegaiwa mashine 16 na wilaya ya Maswa mashine 9 ili kuwasaidia wakulima hao.
Aliongeza kuwa changamoto ya uhaba wa mashine bado inawakabili wakulima hao, kwa mfano kijiji cha Ng’hoboko kina mashine 3 za kupandia wakati huo kina zaidi ya wakulima 100.
Post A Comment: