Msajili Mkuu wa Mahakama Catherine Revocati akielezea jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano wao na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Juma (wapili kutoka kulia) leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama Hussein Kattanga na Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali.
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria itakayofanyika Februari
Mosi mwaka huu.
Hayo yameelezwa
leo jijini Dar es Salaam na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma
alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maonesho ya maadhimisho ya
Wiki ya Sheria nchini yenye maudhui ya ‘Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa
wakati na kwa kuzingatia maadili’.
“Kila mwaka
Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria ambayo huashiria kuanza rasmi
kwa shughuli za Mahakama, kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafunguliwa rasmi na
Rais Magufuli katika viwanja vya Mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar
es Salaam,” amesema Jaji Mkuu Juma.
Jaji Mkuu amesema
kuwa kabla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Mahakama ya Tanzania
pamoja na wadau muhimu katika Sekta ya Sheria watatumia siku tano kuanzia
tarehe 27 hadi 31 Januari mwaka huu kwa ajili ya kufanya maonesho yatakayotoa
elimu kwa wananchi watakaopata nafasi ya kuhudhuria katika viwanja vya Mnazi
Mmoja vilivyopo jijini humo.
Maonesho
hayo yatatanguliwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria
yatakayofanyika Januari, 28 mwaka huu ambayo yataongozwa na Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yatakayoanzia katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo Rais
Mstaafu Kikwete atazindua rasmi Wiki ya Sheria.
Aliongeza
kuwa Wiki ya Sheria inatoa nafasi nzuri kwa wananchi kuzifahamu shughuli
mbalimbali zinazofanywa na Mahakama pamoja na wadau wa sekta ya sheria ili
kufanikisha maboresho endelevu ya Mahakama.
Aidha, Jaji
Mkuu Juma amewahakikishia wananchi kuwa Mahakama itaendelea kupokea malalamiko
na mawazo kutoka kwa wananchi na kuyafanyia kazi hata baada ya Wiki ya Sheria
kuisha.
Wiki hiyo ya
Sheria itaenda sambamba na uzinduzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama
yaliyokamilika yakiwemo ya Mahakama ya Mwanzo Kawe, Kituo cha kisasa cha
mafunzo Kisutu pamoja na Mahakama ya WIlaya ya Bagamoyo, Mkuranga na Kigamboni.
Wadau
wengine watakaoshiriki katika wiki ya sharia pamoja na Tume ya Utumishi wa
Mahakama, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Taasisi ya Mafunzo ya
Uanansheria kwa Vitendo Tanzania, Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha
Mawakili Tanganyika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Jeshi la
Magereza, Jeshi la Polisi, na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi
ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
|
Post A Comment: