Muuguzi mkuu kitengo cha tiba na matunzo(CTC) hospitali ya wilaya ya Chato,Zaina Mussa akitoa maelezo mbele ya waandishi wa habari kwenye chumba cha kutolea dawa. |
Bw Paul Kanyange,mkazi wa chato akielezea namna ambavyo amekuwa akitumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi mbele ya waandishi wa habari. |
|
Waandishi wa habari wakiwa kwenye kikao na Mganga mkuu wa wilaya ya Chato,Atnas Ngambakubi . |
Muuguzi mkuu kitengo cha tiba na matuzo(CTC) hospitali ya wilaya ya Chato,Zaina Mussa akionesha eneo ambalo linatumika kutunza kumbukumbu kwa waandishi wa habari.
Na,Joel Maduka,Chato.
|
Uongozi wa Hospitali ya wilaya ya Chato mkoani Geita , wamelipongeza Shirika lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI kutokana na kutekeleza miradi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa wateja kutokana na mafunzo mbali mbali ambayo yanatolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari Mganga mkuu wa wilaya ya Chato,Atnas Ngambakubi, alisema shirika la AGPAHI limekuwa na misaada mikubwa kwenye vituo vya tiba na matunzo(CTC) ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa semina kwa watumishi ambazo zimeendelea kuwajengea uwezo wa utendaji kazi wa kila siku.
“AGPAHI wamekuwa na msaada mkubwa zaidi ya mapambano ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ikiwa ni pamoja na kutupatia mashine ya kupima wingi wa virusi vya Ukimwi kwa wanaotumiwa dawa, lakini pamoja na kwamba tuna mashine tuna sampo ambazo tumekuwa tunazisafirisha kupeleka Bugando na gharama zote zinalipiwa na AGPAHI”. Alisema Dkt Ngambakubi.
Ameendelea shirika hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundo mbinu kwenye baadhi ya vituo vya afya kumi na tatu (13) na kwenye maeneo ya zahanati, maeneo ya kutolea dawa pia wameweza kuyaboresha.
Pia alisema waanaamini kuwa fedha ambazo zinatolewa na shirika hilo ni za muhimu kwani wilaya bado inauhitaji mkubwa wa ufadhili huo ,pia alisisitiza endapo wafadhili wakasitisha ufadhili huu wananchi watakosa huduma muhimu sana za afya, kwa sasa wanajitahidi kuendelea kujiimarisha na kutenga kiasi cha kutosha kwenye bajeti ya wilaya.
Aidha kwa upande wake Dkt.Zaina Mussa alisema katika hospitali ya wilaya ya Chato, wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wateja kutokuja kwenye matibabu kwa maana ya kufuatilia dawa hali ambayo inabidi watu anayeishi na Virusi vya Ukimwi (MVIU) mshauri kuwafatilia kwa ukaribu ili kuweza kuwarudisha kwenye dawa .
“Unakuta una watoro wa dawa tisini na tano kwa hiyo MVIU mshauri anawafuatilia kwa kuwapigia simu ili waweze kuja kwa ajili ya kupata dawa.Wateja wengine wameendelea kuwa na tatizo la kuendelea kujinyanyapaa mwenyewe” Alisema Zaina.
Moja kati ya watu ambao wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ,Bw Paul Kanyange alisema kwa sasa wameendelea kupata huduma nzuri na pia wanapatiwa madawa kwa haraka zaidi ambapo ni tofauti na zamani wakati shirika hilo likiwa bado alijaanza kufadhili baadhi ya huduma.
“Kwa kweli tunalishukuru sana Shirika la AGPAHI kwa kutuletea huduma hii ya madawa maana imetusaidiakwa kiasi kikubwa kupata dawa kwa urahisi zaidi lakini pia kuchukua tahadhari ya kuhakikisha tunaepukana na maambukizi mapya",alisema Kanyange.
AGPAHI ni shirika la kitanzania lisilo la kiserikali linajishughulisha na programu za kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa watoto, matunzo na huduma za matibabu kwa watu wanaoishi na VVU nchini Tanzania.
Kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wahisani, shirika limekuwa likiunga mkono utoaji wa huduma za VVU katika mifumo iliyopo.
AGPAHI imejikita katika kutoa msaada wa huduma zenye ubora wa hali ya juu na kuhakikisha jitihada za kufikia lengo la pamoja la kutokomeza Maambukizi ya VVU kwa watoto linafikiwa.Shirika linafanyakazi katika mikoa ya Tanga, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, Simiyu.
Post A Comment: