Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu ,
watendaji wa Sekta ya Afya na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya Mkoani humo
wakifuatilia mada mbalimbali katika kikao cha tathmini ya mchango wa wadau
mbalimbali wa Afya Mkoani Simiyu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka wadau na mashirika mbalimbali wanaofanya
kazi na Mkoa huo katika sekta ya Afya
kuelekeza fedha zao zaidi katika masuala yanayojibu mahitaji ya wananchi wa
Mkoa huo kwenye Afya badala ya kujikita zaidi katika kugharamia mafunzo na semina
kwa watumishi.
Mtaka
ameyasema hayo katika kikao kilichofanyika Februari 26, Mjini Bariadi kwa lengo
la kufanya tathmini ya mchango wa fedha za wahisani na wadau mbalimbali wa
sekta ya Afya mkoani Simiyu na matokeo
yake katika mahitaji halisi ya Kiafya kwa wananchi.
Mtaka amesema mkoa huo una wadau wengi wanaounga
mkono juhudi za Serikali katika sekta Afya na wanatoa fedha nyingi ambazo
zikiwekwa pamoja na fedha zinazotengwa na Serikali kupitia bajeti za
Halmashauri zinaweza kujibu mahitaji ya mkoa huo ambayo ni pamoja na upungufu wa zahanati na vituo vya
Afya.
“Msingi mkubwa wa kikao hiki ni kutaka tufanye
tathmini ya fedha zinazotolewa na wadau ndani ya mkoa wetu, kwa mwaka huu kwenye Halmashauri zetu tumetenga
Bilioni 33.4 na tuna shilingi bilioni 11
kutoka kwa wadau kwa ajili ya sekta ya
afya, hivi ‘impact’(matokeo) ya hizi bilioni 11 iko wapi? Natamani hapa kila
mwenye fedha yake atuambie mwaka huu atafanya nini” alisema Mtaka.
“Nashukuru TAMISEMI mko hapa hili ni la kuliangalia
, kama tunaingia mikataba ya shilingi bilioni 11 kwa mwaka na mashirika
yanayofanya kazi za Afya ndani ya Mkoa kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi,
uhamasishaji na semina, wakati tukiwa
kwenye mazingira ambayo hatuna hata nusu ya idadi ya zahanati na vituo vya afya
vinavyohitajika ni lazima tutafakari wote”
alisisitiza Mtaka.
Wakati huo huo Mtaka ametoa wito kwa wataalam wa
Afya kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kuzingatia uzazi wa mpango
na akasisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wazazi watarajiwa (vijana) ili waanze
kufanya maandalizi mapema juu ya maamuzi ya idadi ya watoto watakaoweza
kuwahudumia baadaye.
Naye Katibu Tawala Mkoa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini
amesema malengo waliyojiwekea katika kikao hicho ni pamoja na kuhakikisha kazi
zinazofanywa na wadau wa Afya mkoani humo zinajibu matatizo ya Wanasimiyu na namna ya kuwa na uratibu mzuri wa shughuli zao, mambo ambayo yamepokelewa na
wadau hao na kuahidi kuweka uratibu mzuri ili kuimariasha afya za wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirikala Cuso
International Tanzania, Ndg.Romanus Mtung’e amesema wadau wa Afya Mkoani humo
watashirikiana na Viongozi na Wataalam wa Afya katika kuweka mipango ya baadaye
na watazingatia vipaumbele ambavyo vitaleta matokeo chanya yanayoonekana kwa
wananchi mkoani humo.
Kikao cha wadau wa Afya na Viongozi Mkoa Simiyu
kimewahusisha Viongozi na Wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wakurugenzi
wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Viongozi wa Dini pamoja na
wadau(mashirika) wa Afya wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu wakiwemo AMREF,
AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, PSI,Red Cross, ICAP, TAMA,
INTRAHELTH, WORD VISION, BORESHA AFYA, CHAI, MARIESTOPES na BRIDGE2 AID.
|
Post A Comment: