Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza wakati wa kikao na wawakilishi wa Kampuni ya OreCorp Tanzania Limited (hawapo pichani) walipokutana kwenye Ofisi za Afisa Madini Mkoa wa Geita. |
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mbele katikati) akizungumza na wawakilishi wa Kampuni ya Ore Corp Tanzania Ltd. |
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amezikumbusha Kampuni za Madini nchini kuhakikisha suala la mahusiano na jamii linapewa kipaumbele ili kuboresha utendaji wa shughuli zao.
Amesema hayo Machi 5, 2018 Mkoani Geita alipokutana na wawakilishi wa Kampuni ya OreCorp Tanzania Limited yenye Leseni ya Utafiti ambayo inatarajia kuanzisha shughuli za uchimbaji mkubwa wa dhahabu kwenye eneo la Nyanzaga, Wilayani Sengerema.
Katika mkutano huo uliofanyikia kwenye Ofisi za Madini, masuala mbalimbali ya shughuli za uchimbaji madini yalijadiliwa na msisitizo ukiwa kuhakikisha suala la uboreshaji wa mahusiano na jamii zinazozunguka miradi linapewa kipaumbele.
Biteko alisema uboreshaji wa mahusiano na jamii ni kwa faida ya kampuni kwani kufanya hivyo kutasaidia kuepuka migogoro isiyo ya lazima na hivyo kuboresha utendaji kazi na kuwa na uzalishaji wenye tija.
Aidha, awali kabla ya kukutana na kampuni hiyo, Biteko alikutana na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba na Afisa Madini Mkoa wa Geita, Mhandisi Ally Maganga.
Naibu Waziri Biteko atahitimisha ziara yake hapo baadaye leo hii Machi 6, 2018 kwa kutembelea machimbo ya dhahabu ya Nyang'wale na kuzungumza na wachimbaji kwenye machimbo hayo.
Post A Comment: