Na,Bathromeo Chiwiko,Geita
Halmashauri ya wilaya ya Geita imefanikiwa kugawa vyandarua vyenye viuwatilifu 131,445 kwa uwiano wa chandarua kimoja kwa watu wawili kwa jumla ya kaya 467,609 katika harakati za kutokomeza ugonjwa wa malaria ambao bado ni tishio kwa eneo la kanda ya ziwa.
Akiongea wakati wa kikao cha kutathimini hali ya malaria wilayani hapa kaimu mratibu wa malaria wilaya ya Geita ndugu Fredy Mwaipaja amesema Maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asilimia 16.3% mwaka 2016 hadi 15.1% mwaka 2017 kwa wagonjwa 112,134 sawa na asilimia 36.5% kati ya wagonjwa 310,251 waliofika katika zahanati na vituo vya afya ambao ni wagonjwa wa nje maarufu kama OPD .
Utafiti wa malaria uliofanyika mwezi Oktoba, 2017 katika shule 5 za Msingi Halmashauri ya wilaya Geita unaonyesha wanafunzi 396 kati ya 674 sawa na asilimia 58.8%ya wanafunzi waliopimwa waligundulika na vimelea vya Malaria hali iliyopelekea Halmashauri kuja na mkakati mwingine wa kuhakikisha vyandarua vyenye viwatilifu vinagawiwa shuleni na pia watoto wanafundishwa mbinu mbalimbali za kupambana na Malaria.
Mwaipaja ameeleza kiwango cha upimaji wa malaria kimeongezeka kutoka asilimia 91.8% mwaka 2016 hadi asilimia 98.8% mwaka 2017 na watu waliogundulika wana malaria walipatiwa tiba.
Akilezea Sababu zinazochochea maambukizi ya malaria katika jamii ni pamoja na tabia ya jamii kuchelewa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya utambuzi na kupata tiba ya malaria, Kutumia dawa bila kupima, kutokamilisha dozi kwa wagonjwa wa malaria, Matumizi yasiyo rasmi ya vyandarua kwa shughuli zisizokusudiwa pamoja na Kugomea shughuli za unyunyiziaji wa dawa ya ukoko majumbani”.
“Katika kuhakikisha Malaria inaondoka kabisa Geita kwa sasa tunatoa elimu kwa jamii na tunahakikisha matumizi salama na sahihi ya vyandarua yanatelekezwa na ndio maana tumeamua kugawa vyandarua hivyo kwenye ngazi za shule za msingi kama njia mojawapo ya kuzuia malaria” Ameongeza Mwaipaja.
Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita baina ya Wataalam kutoka Halmashauri ya wilaya ya Geita pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ya “Tanzania Communication and Development Center”(TCDC),Pamoja na New Light Children Organisation (NELICO) kwa lengo la kutathimini hali ya Ugonjwa wa Malaria wilayani hapa.
Post A Comment: