Na Stella Kalinga, Simiyu
Kaya 6120 sawa na asilimia 52 ya walengwa wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri
ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu zimewezeshwa kulima pamba ekari 8712 katika
Msimu wa mwaka 2017/2018 kwa kutumia fedha za uhawilishaji.
Hayo yalibainishwa na
Mratibu wa TASAF Mkoa wa Simiyu Bw. Nyasilu Ndulu wakati
wa kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi juu ya
mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.
Nyasilu
amesema pamoja na kulima pamba walengwa wa mpango huo katika Wilaya ya Bariadi
na wilaya nyingine Mkoani Simiyu, kupitia fedha za uhawilishaji (wanazopewa)
wamefanikiwa kujenga nyumba, kufuga, kuanzisha biashara ndogo ndogo na kujiunga
na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF).
Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa zoezi la
uhawilishaji chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini awamu ya tatu mwaka 2015
hadi sasa, tayari awamu 17 za
malipo zimekwisha fanyika kwa walengwa 37, 533 na jumla ya shilingi bilioni
28.9 zimelipwa kwa wahusika.
Amesema fedha hizo
zimejumuisha ruzuku za aina mbili ikiwa ni ruzuku ya msingi na ile itokanayo na
utimizaji wa mashati ya Afya na Elimu ambapo watoto 39,068 sawa na asilimia
90.3 wameweza kupata mahitaji muhimu ya shule na kukuhudhuria shuleni na watoto
51, 280 sawa na asilimia 93.1 wamepata mahitaji ya kliniki na kupelekwa
kliniki.
“Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeweza
kuwasaidia walengwa kujikwamua kutoka kwenye umaskini, wapo walioanzisha
biashara, wanaolima, wanaofuga, waliojenga nyumba bora; kwa kutumia fedha hizi
wanazopewa wapo ambao watoto walikuwa hawahudhurii shuleni na kliniki lakini
sasa hivi mahudhurio mazuri” Alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka awali akifungua kikao amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata walengwa, wanufaika
wote waliofanya mambo ya maendeleo ni vema wakawa mfano kwa wenzao
huku akiwataka wale walioshindwa kuondolewa kwenye mpango huo.
Aidha, Mtaka aliwataka walengwa
wote wa mpango kuendana na malengo ya nchi ya kuelekea kwenye Uchumi wa Kati
ifikapo mwaka 2025 badala ya kuwaza kuendelea kubaki katika mpango huo.
“Mtazamo wangu mimi ni vizuri wanufaika
wa TASAF waendane na Mpango wa Nchi, tunaposema tunataka kwenda kwenye Uchumi
wa Kati kufikia mwaka 2025 wanufaika wa TASAF wanapaswa kujindaa kwenda kwenye
uchumi wa kati, ili badala ya watu kutaka tu kuingia kwenye mpango, tupate watu wanaotaka kutoka baada ya kupiga
hatua na kutoka kwenye umaskini waliokuwa nao mwanzo” alifafanua Mtaka
Nae Bw. Fariji Mishael mtaalamu wa
ufuatiliaji wa tathmini kutoka Ofisi ya TASAF Makao makuu aliupongeza Mkoa wa Simiyu kwa
kutekeleza mpango huo vizuri na kuomba wataalamu kuwasaidia walengwa walio
kwenye maeneo yao katika kuwashauri
namna bora ya kuendesha miradi waliyoianzisha ili iwe endelevu na iweze
kuwasaidia kiuchumi.
Post A Comment: