Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaja mikoa ya
Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa
sekondari.
Waziri mkuu pia ameitaja mikoa ya Rukwa, Geita,
Tabora, Singida na Simiyu kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa shule za
msingi.
Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa ameitaja
mikoa hiyo leo Jumatatu Aprili 2,2018 akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika
uwanja wa Magogo mkoani Geita.
Mbio za Mwenge zitakazohitimishwa Oktoba 14,2018
mkoani Tanga zinaongozwa na kauli mbiu “Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa
kwa maendeleo ya nchi yetu.”
Majaliwa amesema Mkoa wa Tabora unaongoza kwa
asilimia 9.7 ya wanafunzi watoro wa sekondari ukifuatiwa na Geita (asilimia
8.1), Mtwara (asilimia 6.1) na Shinyanga (asilimia 6.3).
Kwa shule za msingi, Rukwa inaongoza kwa asilimia
3.2, ukifuata Geita (asilimia 3.1), Tabora (asilimia 2.9), Singida (asilimia 2)
na Simiyu (asilimia 2).
“Kwa jumla utoro wa wanafunzi wa sekondari ni mkubwa
kuliko shule za msingi. Naikumbusha mikoa yote niliyoitaja kuhamasisha wananchi
wakiwamo wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu
shuleni kwa kutumia utaratibu wa sheria zilizowekwa,” amesema Majaliwa.
Aidha , Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Walemavu Mheshimiwa Jensita Mhagama ameelezea kuwa mwenge ni Chombo
kilichoasisiwa na Baba wa Taifa ,Mwl Julius Kambarage Nyerere Mwaka 1961 ikiwa
ni tunu na ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika.
“Mbio za mwenge wa uhuru zilianza rasimi mwaka 1964
baada ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar uliozaa nchi inayoitwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania”Alisema Waziri Jenista.
Mwenge wa uhuru utakimbizwa katika mikoa yote 31 ya Tanzania katika halmashauri 195 na kwa muda wa siku 195.
Sherehe hizo zilizosindikizwa na burudani mbalimbali
zikiwemo ngoma za asili, kwaya, na halaiki zilifana huku zilihuidhuriwa na
wakazi wengi.
Huku kauli mbiu ikiwa ni” Elimu ni ufunguo wa maisha
,wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa”
Post A Comment: