ZAIDI YA BIL 40 KUTUMIKA KUJENGA MTAMBO WA KUPOZA UMEME GEITA

Share it:


Serikali kupitia wizara ya Nishati imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 40 ambazo zitatumika kujenga mradi wa kituo cha  kupozea umeme (Sub-sitation) kwenye mtaa wa mpovu kata ya Mtakuja Mkoani Geita.

Kituo hicho kitasaidia kusambaza umeme kwenye maeneo mbali mbali yaliyomo Mkoani humo na mikoa jirani na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mega wat 98  ambapo kwa sasa Mkoa huo unatumia mega wat 8.

Akizungumza  hapo jana wakati alitembelea eneo ambalo linatarajia kuwekwa mradi huo,Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alisema mkandarasi ambaye anajenga mradi huo ni kampuni ya CAMCE  na kufikia mwezi mei mwakani mradio huo utakuwa umekamilika kutokana na kasi ambayo mkandarasi atatakiwa kwenda nayo.

Hata hivyo Waziri Kalemani amewataka wananchi kutunza miundo mbinu ya umeme huo kutokana na gharama kubwa ambazo zimekuwa zikitumika kuwekeza  mitambo hiyo.

“Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali kutupa pesa za walipa kodi kwaajili ya mradi huu na jambo jingine la kuendelea kumshukuru Rais ni kwamba tumekwisha kukamilisha malipo ya awali kwa watu wenye maeneo haya kwa maana kwamba tumeshalipa fidia kwa hiyo kazi imebaki kwa mkandarasi kuhakikisha kuwa anafanya kazi na mchana hili kazi hii iweze kukamilika”Alisema Waziri Kalemani.

Mbunge wa Jimbo la Geita mjini ,Constatine Kanyasu alisema kuwa anaipongeza serikali kwa namna ambavyo imeweza kusikia kilio cha wananchi wa Geita kwani ni muda mrefu walikuwa wakilia na tatizo la kukatika mara kwa mara umeme na kwamba kupitia mtambo huo tatizo hilo litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huo,Mhandisi Robert Gabriel aliwataka wafanyabiashara kuja na kuwekeza mkoani humo viwanda mbali mbali kwani umeme ambao unawekwa utakuwa ni wa uhakika na utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli zao zikiwemo za uchenjuaji wa madini na kwamba ni wakati  wao wakuchangamkia fursa ya kuendelea kutanua wigo wa kuwekeza.

“Mheshimiwa Waziri kwa sasa sisi kazi yetu kubwa ni kuendelea kuwataka wawekezaji waje waweze kuwekeza viwanda na niwahakikishie wananchi tu kwamba kwa sasa tutaondokana na tatizo la kukatika katika kwa umeme hivyo mimi ninawakaribisha waje waweze kuwekeza kwenye mkoa wetu wa Geita na tunaamini kuwa kwasasa tutanufaika kutokana na mapato ambayo yataweza kuingia kwa haraka zaidi kwani kila kitu kitakuwa sawa”Alisema RC Gabriel.

Pia kwaupande wake,Hamis Mwananyanzala ambaye ni mchimbaji mdogo aliishukuru serikali na kwamba wanaamini wao kama wachimbaji wadogo wataweza kunufaika na mradi huo wa umeme kwani hapo awali walikuwa wakipata shida kutokana na nguvu ya umeme kuwa  ndogo.


Waziri wa nishati Dkt,Medard Kalemani anaendelea na ziara yake ya siku mbili mkoani humo yenye lengo la kutatua kero ya umeme kwa wananchi.

Share it:

habari

Post A Comment: