Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited
(MeTL Group), Mohammed Dewji akizungumza katika mkutano wa Global
Business Forum 2017 kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika, mkutano huo wa
siku mbili umefanyika Dubai, UAE na kuhudhuriwa na watu 5860 wakiwepo
viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wafanyabiashara(Picha na Clouds Media)
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises
(MeTL Group), Mohammed Dewji amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.
Dewji ametoa
pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business
Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za
Kiarabu (UAE).
Mfanyabiashara
huyo ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni
mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa
kati.
Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea
kushirikiana na serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha
anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo litasaidia kukuza
uchumi wa nchi na kwa wananchi..
“Nianze kwa kumpongeza Mhe. Rais John Pombe
Magufuli kwa shabaha yake ya viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani
lakini pia watu wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi ambazo
zitaisaidia serikali kuwekeza kwenye mambo ya afya na maji na huduma za jamii.
Mimi shabaha yangu kwenye miaka saba au nane ijayo MeTL Group tunataka tuajiri
watu 100,000,” alisema Dewji.
Dewji ambaye
kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini aliongeza kuwa
utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha
miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa sana.
“Mimi naona
kwa kasi ya Mhe. Rais kwenye miaka miwili au mitatu ijayo tutakuwa tumefika
mbali sana, uchumi wetu kwasasa ni asilimia sita au saba lakini kama tukitaka
kuondoa umaskini lazima nchi yetu ukuaji wa uchumi uanze kukua kwa zaidi ya
asimilia 10, mimi nina muamini sana Mhe. Rais na shabaha yake kwahiyo Mungu
atutangulie na sisi tupo nyuma yake tutafika hivi karibuni,” alisema Dewji.
Pia Dewji
alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa
mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na
wawekezaji alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia
amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo
hapa nchini.
“Umuhimu ni
mkubwa sana nakuja hapa kama MO lakini pia nawakilisha nchi yangu Tanzania,
nimeitangaza nchi yangu ili watu waje na wawekeze, nimewaeleza mazingira yetu
ya uwekezaji ni mazuri, tuna malighafi na tunahitaji viwanda angalau watu wetu
wa Tanzania wapate ajira na serikali ipate kodi,” aliongeza Dewji.
|
Post A Comment: