Mkuu wa Wilaya ya Chato iliyopo
mkoani Geita, Shaban Ntarambe amekiri kuwa ushirikiano wa shirika la
Plan International katika kudhibiti ajira hatarishi za watoto
umefanikiwa kumaliza tatizo hilo katika Kijiji cha Msasa.
Hayo ameyasemwa wakati alipokuwa akizungumza na mtandao huu juu ya mchango wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa
Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na
kuratibiwa na shirika la plan International jinsi ulivyowasaidia
wananchi wa Kijiji hicho.
Ntarambe amesema kuwa ushirikiano
wa Shirika hilo, jamii pamoja na uongozi wa migodi iliyopo kwenye
Kijiji hicho umesaidia katika kuhakikisha elimu ya ajira, afya na
usalama kwa watoto inatolewa, hivyo kupitia elimu hizo wananchi wamepata
uelewa juu ya athari za ajira za watoto na kujumuika katika uzuiaji wa
ajira hizo.
“Tumefanikiwa kwa asilimia zote
kuzuia ajira za watoto katika eneo hilo ambalo lina mkusanyiko mkubwa wa
wachimbaji wa madini, kimsingi ni kwa sababu ya ushirikiano unaotolewa
na shirika la Plan International kwani wanatoa rasilimali nyingi
zinazowezesha kufanikisha kuondoa tatizo hilo”, alisema Ntarambe.
Akiongea kuhusu suala la athari
wanazopata watoto wadogo wanaobebwa na mama zao wanaofanya kazi migodini
amesema kuwa wanasaidiana na shirika hilo katika kuwapatia elimu
pamoja na mitaji ili waachane na kazi za migodi na badala yake watafute
kazi mbadala za kujitafutia vipato ili kuwakinga watoto wadogo
wasiathiriwe na kazi zinazofanyika katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Mratibu wa
Mawasiliano wa Shirika hilo, Raymond Kanyambo amemshukuru Mkuu wa Wilaya
hiyo kwa kutambua umuhimu wa shirika hilo na kuahidi kuendelea
kushirikiana nae katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa
wilaya hiyo haswa katika masuala ya unyanyasaji wa watoto na ukatili
unaofanywa kwa wanawake.
“Shirika letu linahusika na
kutetea haki za watoto, hivyo tuliona ni vyema kupeleka nguvu zetu katika maeneo yenye migodi kwa kuwa ni maeneo yanayoongoza katika utoaji
wa ajira za watoto walio na umri chini ya miaka 18, mradi huu
ulitekelezwa katika wilaya za Nyan’ghwale na Geita lakini baada ya kuona
mafanikio tumeamua kuiongeza wilaya ya Chato ili kukomesha kabisa
tatizo hili”, alisema Kanyambo.
Mradi huu wa miaka mitatu una
lengo la kuondoa ajira hatarishi na vitendo vya ukatili kwa watoto
wanaoishi karibu na maeneo ya migodi, umeanzishwa Novemba 2015 na
utagaharimu jumla ya Euro 1,500,000 hadi kuisha kwake.
Post A Comment: