Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mbungu wa Jimbo la Dimani Fumba, Zanzibar,
Mheshimiwa Hafidh Tahir Ali aliyefariki dunia kwenye Hospitali Kuu ya
Dodoma usiku wa kuamkia leo Novemba 11, 2016.
TFF ilijulishwa kifo cha
Mheshimiwa Hafidh na Mbunge wa Jimbo jipya la Ulyankulu, Wilaya ya
Kaliua mkoani Tabora, John Kadutu ambaye alisema leo walikuwa na
programu ya kusafiri kwenda Tabora kushiriki mazishi ya Mbunge wa zamani
wa Urambo, Samwel Sitta lakini kabla ya kwenda mazoezi alfajiri,
waliarifiwa kuhusu kifo hicho. “Inasikitisha, lakini ni ya Mungu yote,”
alisema Kadutu.
Kifo hicho kimemsikitisha Rais
Malinzi ambaye alituma salamu za pole na rambirambi kwa Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akisema taifa limepata
msiba mwingine mzito kwa Mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa mpira wa
miguu aliyekuwa anatambuliwa/kuwa na beji ya Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA).
Hakika alikuwa kiongozi wa karibu
na watu hasa kutokana na michezo ambayo siku zote alikuwa akiota ndoto
za kuifikisha mbali hasa ukirejea kuwa ni jana tu Novemba 10, mwaka huu
alichaguliwa na wanachama wenzake wa Young Africans – tawi la Bunge
kuwa Katibu wa tawi hilo chini ya Mwenyekiti Venance Mwamoto – Mbunge wa
Kilolo mkoani Iringa.
Ukaribu huo na watu ndio
uliompaisha wakati fulani kuwa mmoja watangazaji mahiri wa redio
alipoganya kazi hiyo na manguli wengine kama David Wakati kabla ya kuwa
Msemaji wa Serikali ya Awamu ya Tano ya SMZ kabla ya kuwa Mbunge wa
RahaLeo.
“Wiki hii imekuwa ngumu kwangu,
tumepoteza viongozi wa mfano na wanamichezo mahiri katika kucheza
michezo hususani mpira wa miguu na kuuongoza hata kama ni kwa mawazo yao
chanya tu. Mheshimiwa Hafidhi ni sehemu ya wanamichezo hao mahiri, ni
pigo kubwa hasa kwenye tasnia ya mpira wa miguu. Dua zetu ni Mwenyezi
Mungu amghufie na kumrehemu marehemu,” alisema Malinzi.
Katika salamu zake za rambirambi,
Rais Malinzi pia alitoa pole kwa familia ya marehemu Hafidh Tahir Ali,
ndugu, jamaa, majirani, na marafiki hususani wapiga kura wa Jimbo la
Dimani Fumba kwa kumpoteza kiongozi wao hivyo kuwataka kuwa watulivu
wakati huu mugumu kwao.
Pia Rais Malinzi amesema vifo cha
Sheikh Said Mlohammed, Mzee Mheshimiwa Sitta na Mheshimiwa Tahir,
vibaki kuwa sehemu ya funzo kwetu katika kujiandaa na maisha ya baadaye
kwa sababu zote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
Post A Comment: