Mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge
la 9 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samuel Sitta unatarajiwa
kuagwa leo mchana na wabunge wa Bunge hilo katika viwanja vya Bunge vya
mjini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa mjini hapo
na Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alipokuwa akitoa ratiba ya kuuaga
mwili wa spika mstaafu itakayoanza mara baada ya kumalizika kwa shughuli
za Bunge za kipindi cha asubuhi.
Mhe. Ndugai amesema kuwa Bunge
linatarajia kuupokea mwili wa mpendwa huyo leo mnamo majira ya saa 8
mchana kutoka katika uwanja wa ndege wa Dodoma na kupelekwa moja kwa
moja ndani ya Bunge hilo kwa ajili ya kupewa heshima za mwisho na
wabunge.
“Baada ya mwili wa mpendwa wetu
kuwasili katika viwanja hivi, tutakuwa na kikao maalum cha Bunge
kitakachofanyika mida ya saa 8:30 mchana ambapo wabunge watapata nafasi
ya kutoa salamu za rambirambi na baadaye utaratibu wa kutoa heshima za
mwisho utafuata”, alisema Mhe. Ndugai.
Spika Ndugai ameongeza kuwa baada
ya utoaji wa heshima za mwisho utakaoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa pamoja na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
Mhe. Freeman Mbowe, kwa mwili wa marehemu Samuel Sitta utasafirishwa
kwa ndege mnamo majira ya saa 10 jioni kwenda wilaya ya Urambo, mkoani
Tabora kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Novemba 12 mwaka huu.
Aidha, Mhe. Ndugai amefafanua
kuwa katika msiba huo Bunge litawakilishwa na wabunge 10
watakaochaguliwa na Tume ya Huduma za Bunge kwa kuzingatia uwakilishi wa
vyama ukiongozwa na yeye Spika Mhe. Ndugai kwenda mkoani Tabora kwa
ajili ya mazishi.
Kutokana na msiba huo, Mhe.
Ndugai amesema kuwa Bunge litajenga misingi ya kuwaheshimu viongozi wa
kitaifa wanaopatwa na jambo la namna hiyo kwa kupewa heshima hizo za
kuletwa Bungeni kwa ajili ya kuagwa kwa msingi wa Bunge kuwa ndio nyumba
ya uwakilishi wa Watanzania wote.
Imeandaliwa na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
|
Post A Comment: