Boniface Wambura - Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi
Bodi ya Ligi Tanzania Bara imeziondoa kabisa katika orodha yake timu za Geita Gold Sports na Polisi Tabora kwa kushindwa kuwasilisha usajili wake kwa ajili ya kushiriki ligi daraja la pili msimu huu.
Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Boniface Wambura, amesema maamuzi hayo ni kwa
mujibu wa kanuni za bodi hiyo, ambazo haziruhusu timu kushiriki ligi
yoyote kama itakuwa haijafanya usajili.
Wambura amesema timu hizo zilishushwa daraja na kutakiwa kushiriki ligi
daraja la pili msimu huu, hivyo zilipaswa kuwasilisha majina ya
wachezaji wake kwa ajili ya ligi hiyo lakini hazikufanya hivyo hadi
sasa, kipindi ambacho ligi imekwishaanza.
"Hatuwezi kuacha kucheza ligi eti kwa sababu wao wana kesi, status
waliyonayo ni kucheza ligi daraja la pili, walitakiwa kufanya usajili,
sasa kama timu haijafanya usajili, ni timu gani itacheza ligi?, suala la
review ya kesi yao siyo wao tu hata Oljoro wanasubiri review lakini
walifanya usajili na wanaendelea na ligi" amesema Wambura.
Geita Gold Sports
Kwa upande wa uongozi wa Geita Gold Sports kupitia kwa Seif Kiyunge,
amesema wao kama Geita bado hawajapokea taarifa yoyote ya kufutwa,
isipokuwa wanachojua ni kuwa hadi sasa wanasubiri rufaa waliyoikata ya
kupinga kushushwa daraja isikilizwe, ambapo wanachodai ni mapitio ya
hukumu ya awali
"Wasipokuwa makini watalazimika kutulipa pesa nyingi sana maana bado
mapitio tuliyoomba hayajafanyiwa kazi, na pia TAKUKURU hawajatoa matokeo
ya uchunguzi wa tuhuma za rushwa, kwahiyo endapo itabainika kuwa
hapakuwa na upangaji matokeo, na sisi tumeshafutwa itabidi tudai fidia
kubwa sana ya kufutwa" Amesema Kiyungi.
Ismail Aden Rage - Mlezi wa Polisi Tabora
Kwa upande wake mlezi wa Polisi Tabora Ismail Rage ametupia lawama
Baraza la Michezo kwa kukaa kimya na kwamba kuna mtu anatakiwa
kutumbiliwa kama ilivyokuwa kwa Sepp Blatter wa FIFA.
Post A Comment: