TASNIA YA HABARI YAPATA PIGO

Share it:






Tasnia  ya Habari imepata pigo kubwa la kifo cha Mpigapicha mahiri, Mpoki Bukuku (44) aliyekufa jana kutokana na majeraha ya kugongwa na gari eneo la Mwenge-ITV, Dar es Salaam juzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The Guardian Limited ambako Bukuku alikuwa akifanya kazi, Richard Mgamba alisema katika taarifa yake jana kuhusu kifo hicho kuwa, Bukuku alifariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza kuwa Bukuku alifia katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma wa MOI, Almas Jumaa alithibitisha hayo kupitia taarifa mbalimbali za mitandao ya kijamii.

“Tumepoteza nguzo katika tasnia ya habari. Leo (jana) kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusu kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku”, alieleza Mgamba.

Kwa mujibu wa Mgamba, Bukuku amefariki asubuhi. Mgamba alisema katika familia yake, wamempoteza baba, mume na rafiki wa kweli, na kwa Kampuni ya The Guardian Limited, wamempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari.

“Bukuku alikuwa ni mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa ni mtu aliyeipenda fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine wote ilimuweka matatani,” alisema Mgamba.

Kwa upande wa Chama cha Wapigapicha za Habari Tanzania (PPAT) ambapo Bukuku wakati wa uhai wake alikuwa ni mwanachama na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho, kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho cha ghafla cha Mpigapicha mwenzao.

Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa PPAT, Mroki Mroki, ambaye pia ni Mpigapicha Mwandamizi wa gazeti , alisema ni pigo kubwa kwa chama na wapigapicha wote wa habari nchini, kwani uzoefu wake katika kazi ulikuwa ukihitajika sana na wapigapicha chipukizi kujifunza.
Share it:

habari

Post A Comment: