Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi
Mhe. William Lukuvi amevifutia hatimiliki viwanja 15 vilivyokuwa
vinamilikiwa na raia mmoja wa Uingereza ambapo serikali imevitaifisha
viwanja hivyo vilivyopo katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Viwanja hivyo vilivyokuwa
vinamilikiwa na Mfanyabiashara maarufu jijini hapa, Hermant Patel,
mwenye uraia wa Tanzania na Uingereza kitendo ambacho ni kinyume na
taratibu na sheria za nchini zinazozuia raia wa kigeni kumiliki ardhi.
Aidha, Mhe. Lukuvi amesema
anayeruhusiwa kumiliki ardhi nchini ni raia wa Tanzania pekee na
kuongeza kwamba kwa watanzania waishio nje ya nchi na kuukana uraia wao
nao hawataruhusiwa kumiliki ardhi bali watapewa ardhi kama ilivyo kwa
wawekezaji kutoka mataifa mengine.
Mhe. William Lukuvi amesema mtu
akishaukana uraia wa Tanzania hana haki tena kama raia wa Tanzania,
hivyo ataruhusiwa kumiliki ardhi kama mwekezaji tu na siyo kama raia wa
Tanzania. Lukuvi amesisitiza kuwa ardhi itabaki kuwa ya Watanzania tu na
ameagiza mamlaka zota kutawasaka wale wote ambao wanamiliki ardhi
kinyume na sheria za nchi.
Uamuzi wa kufuta hatimiliki hizo
ulitolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi wakati
akizungumza na wanahabari juu ya hatua hiyo ya Serikali ya kuvifuta hati
hizo jijini Mwanza.
Lukuvi alisema kuwa awali
Serikali ilikuwa ikifahamu mfanyabiashara huyo anahatimiliki ya viwanja
vitano lakini baada ya uchunguzi uliohusisha Taasisi ya Kuzia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza wamebaini raia huyo
anamiliki viwanja 15.
Alisema kuwa kitendo cha
mfanyabiashara huyo kumiliki, viwanja 15 katika mikoa ya kanda ya ziwa
kwa njia ya udanganyifu kumeonesha ni namna gani raia wa kigeni
wasivyokuwa waaminifu na kuwakanya kuacha mchezo huo.
“Viwanja hivi tumevitaifisha na
sasa vimerudi chini ya Serikali na baada ya hapo vitapigwa mnada,
hatutakubali kuona watu ambao sio wazawa wakilimiki ardhi kiasi hicho.
“Huyu Patel (Hermant Patel)
alikuwa na pospoti (hati za kusafiria) mbili za Tanzania na Kenya hiyo
imeonesha ni namna gani alivyotapeli na wale wote wenye paspoti mbili
wakae chonjo,” alisema Lukuvi.
Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa
Isimani mkoani Iringa, alisema kuwa wizara ya ardhi ni miongoni mwa
wizara zinazotumika kupitisha utakatishaji wa fedha haramu huku akidai
raia wengi wa kigeni wanaonunua ardhi hutakatisha fedha chafu.
Hata hivyo, alisema kuwa baadhi ya
watumishi katika wizara yake wameonekana kutokuwa makini katika
usimamizi mzuri wa utoaji wa hati za umiriki arshi kwa raia wa kigeni
kitendo ambacho alikikemea na kuwataka kubadilika.
Baadhi ya viwanja vilivyofutiwa
hatimiliki na kutaifishwa na Serikali ni pamoja na kiwanja namba 98
kitalu ‘ F’ nyakato Mwanza, kiwanja namba 45 Mkuyuni Mwanza, Viwanja
namba 539 na 560 kitalu ‘A’ Magongo Geita.
Vingine ni kiwanja namba 113
kitalu ‘A’ Nyamongoro Mwanza, kiwanja namba 798 Magongo Geita, kiwanja
namba 529 Magogo – Geita, viwanja namba 531 na 532 Bombambili Geita na
viwanja namba 533 na 534 kilichopo Geita.
Viwanja vingine ni kiwanja namba
332 Kilichopo Bwiru Ilemela Mwanza, namba 330 kitalu ‘A’ Bwiru Ilemela
Mwanza, namba 115 Nyamhongoro Mwanza, kiwanja namba 3 kitalu ‘C’
kilichopo Lamadi Busega mkoani Simiyu na kiwanja namba 1 na 2 vilivyopo
Lamadi – Busega mkoani.
Mhe. Lukuvi Ameyasema hayo jana katika ofisi ya Ardhi ya Kanda ya Ziwa iliyopo mkoani Mwanza.
|
Post A Comment: