Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia
mwanzoni mwa Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za
wadaiwa sugu kwenye vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali
vya elimu ya juu kuanzia wale wa miaka 10 iliyopita.
Bodi hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30,
mwaka huu, kwa wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo,
vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika
kulipia gharama za kuwasaka na kuendesha kesi.
Pamoja na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo
iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa
kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi
cha kuhakiki waajiriwa wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa
waliokopa HESLB, na adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36
jela.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa
muda huo wa siku 30 walioutoa, wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa
hawajajisalimisha wenyewe kwa hiari, kulipa madeni yao wataanikwa
hadharani na picha zao.
“Tumeamua kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua
wadaiwa hawa wa bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka
ili waturejeshee fedha zetu,” alisema Badru.
Aidha, alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni
kuutangazia na kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi
wengine kukosa fursa ya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha
iliyopo bado haitoshelezi.
Alisema bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na
baadaye kuwaongezea tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka
huu, hivyo kinachofuata ni utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia
fursa hiyo ya kujisalimisha.
Mkurugenzi huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza
kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa
kushindwa kulipa madeni yao, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni
pamoja na kulipia gharama za usumbufu wa kuwatafuta.
Alisema utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi
zaidi, kupata fursa ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni
vyema wanafunzi wote wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa
muda muafaka uliowekwa kisheria.
Badru alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya
Mikopo, imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na
mikopo kutoka miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga
na kutafuta ajira.
Aidha, alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa
waajiriwa walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya
mishahara yao hadi asilimia 15.
“Tunawashukuru sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija
kwenye sheria hii katika eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato
kifikie hadi asilimia 30 na zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya
wadau wakiwemo wa wabunge walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,”
alisema.
Alisema ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo
hiyo aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi
hiyo imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria
kupitia marekebisho hayo ya sheria.
“Tumeunda kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu
mbalimbali nyeti, kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka
huu, ya kuhakiki kila ofisi ya waajiri sugu ili kubaini kama ama
wamewasilisha majina ya wanufaika wa mikopo hii au wanawakata bila
kuwasilisha michango hiyo kwa bodi,” alisema.
Alisema waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa
kutoisaidia bodi kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato
yao, wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua
makato hayo waliyoshindwa kuyawasilisha na endapo watashindwa
watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha muda wa miezi 36 jela.
“Lakini pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha
wanapeleka wenyewe taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa
makato, yeyote atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye
atawajibishwa,” alisisitiza.
Halikadhalika, Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa
wanufaika wa mikopo hiyo ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo
rasmi wa ajira, ambao nao wanatakiwa kurejesha kiasi kisichopungua Sh
100,000 kila mwezi.
Akizungumzia mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa
sugu kulipa wenyewe madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya
fedha, yameongezeka kutoka Sh bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh
bilioni nane.
Alisema tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza
wenyewe kwa hiari na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote
na wengine wakiyapunguza.
Hadi sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva,
inazozidai kwa wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140
pekee ndio zimelipwa.
Kwa mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179
wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu
ianzishwe Juni, mwaka 1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa
wanafunzi hao.
Jumla ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na
mikopo ya HESLB, wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi
cha Sh trilioni 1.4, baada ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa
sheria kuisha.
|
Post A Comment: