YANGA YAZIDI KUIKIMBIZA SIMBA KATIKA MBIO ZA UBINGWA,YATOA KIPIGO CHA MSIMU KWA NDANDA FC

Share it:

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania timu ya Yanga imeendelea kuifukuzia kimya kimya Simba katika mbio za Ubingwa msimu huu baada ya kuivuruga Ndanda FC kwa jumla ya magoli 4-0 mchezo uliomalizika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Yanga waliingia uwanja huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 na African Lyon na ilipelekea kipindi cha kwanza kulishambulia lango la wageni kama nyuki huku wakitumia mashambulizi ya pembeni kupitia kwa Simon Msuva kulia na kushoto wakimtumia Emmanuel Martin aliyetokea JKU ya Zanzibar.

Haikuwachukua muda wenyeji kupata goli dakika ya nne likifungwa na Donald Ngoma aliyepiga kichwa baada ya kupokea mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima baada ya kuingia bao hilo Ndanda FC waliendelea kupotea katika sehemu ya kiungo iliyokuwa chini ya Salum Telela.

Donald Ngoma alirudi tena kwenye nyavu za Ndanda dakika ya 21 akifunga la pili huku likiwa la saba msimu huu baada ya kupokea pasi toka kwa mchezaji bora wa msimu uliopita Juma Abdul na katika dakika ya 25 mshambuliaji toka Burundi Amis Tambwe alifunga la tatu dakika ya 25 na likiwa goli lake la 9 akimalizia pasi ya Simon Msuva hadi mapumziko wenyeji walikuwa mbele.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko na kwa mara ya kwanza mchezaji toka Zambia Justine Zulu ‘Mkata umeme’aliingia akichukuwa nafasi ya Juma Makapu na kushangiliwa na umati wa mashabiki waliohudhuria katika uwanja wa Uhuru.

Dakika ya 88 Mlinzi mwenye akili ya Mpira na Raia wa Togo huku akiwa na asili ya Ivory Coast Vicent Bossou alifunga goli la nne huku likiwa ni la pili kwake msimu huu akimalizia Mpira wa kona uliopigwa na Juma Abdul hadi mwamuzi anamaliza Mpira Yanga wameibuka na ushindi wa magoli 4-0.

Kwa matokeo hayo Yanga wamebaki nafasi ya pili wakiwa na alama 40 huku wakizidiwa alama moja na Simba wenye alama 41 na wakiwa na mchezo mmoja ambako kesho watashuka dimbani kucheza na Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Uhuru majira ya kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki.


Matokeo mengine ya Ligi Kuu ya Tanzania bara Mtibwa Sugar wameweza kuizamisha Majimaji goli 1-0 bao likifungwa kipindi cha kwanza dakika ya 37 kupitia kwa Jaffar Salum.
Share it:

michezo

Post A Comment: