Wakati Wazanzibari leo wakiadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein (pichani), amebainisha kuwa mapinduzi hayo ndio alama, sifa, ukombozi na uhuru wa raia hao wa visiwa vya Zanzibar.
Dk Shein amesema hana ugomvi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi na kubainisha kuwa wanatofautiana kisiasa, ni jambo la kawaida na mazungumzo ya muafaka yalishafanyika. Pamoja na hayo, Rais huyo amebainisha kuwa anaamini amechaguliwa kihalali na Wanzanzibari, ambapo kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2015, hakukuwa na shinikizo lolote kutoka serikalini bali ni maamuzi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) baada ya kubaini mchezo mchafu kwenye uchaguzi huo.
Akizungumza katika kipindi cha Funguka kilichorushwa na Azam TV jana usiku, Dk Shein alisema kilichohitajika ni mazungumzo ya pande mbili ambayo yalifanyika baina yao na mwelekeo ulikuwa mzuri lakini Maalim Seif hakutaka kurudia uchaguzi.
Mvutano huo ulijitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo hayo na kusababisha mvutano wa kisiasa kabla ya kutangaza kurudiwa Machi 20, 2016, ambao CUF iligoma kushiriki.
Katika mahojiano hayo, Dk Shein alisema, “Mimi nilikuwa mwenyekiti wa mazungumzo yale na Maalim upande wa pili huku wajumbe wakiwa marais wastaafu, Ally Hassan Mwinyi, Aman Karume na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd.
“ZEC ni tume huru na inayojisimamia kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Zanzibar, taasisi yoyote haiwezi kuiingilia hata kama ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ndiyo maana wao (NEC) hawakuona dosari katika uchaguzi lakini ZEC waliziona na kutoa sababu tisa za kufuta uchaguzi,”alisema Dk Shein.
Alisema uchaguzi wa Zanzibar umekuwa na matatizo tangu mwaka 1957 na wa awamu hii, Tume ilikuwa na hoja za msingi kuurudia huku akisema mwenyekiti wa Tume anateuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba na si kwa ajili ya kumpendelea.
Changamoto za Muungano
Dk Shein alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa katika kudumisha Muungano na changamoto zake pekee anazozitambua ni tume ya pamoja ya fedha na suala la mafuta ambalo limepatiwa ufumbuzi.
“Kabla ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa kelele za Muungano na muundo wa Serikali hazikuwahi kusikika lakini baada ya baadhi ya wanaCCM kuenguliwa na kuhamia upande wa pili, ndiyo walioanza kuwalisha watu sumu. Lakini anayeupinga Muungano haijui asili yake,” alisema Dk Shein.
Mchakato wa Katiba
Alipoulizwa kuhusu Katiba mpya baada ya Rais John Magufuli kusema hicho si kipaumbele chake, Dk Shein alisema hayo ni masuala ya kushauriana baina ya viongozi hao wawili.
“Mchakato wa Katiba tuliuanza mimi na Jakaya Kikwete (Rais mstaafu) na ile Katiba ni ya Muungano, hivyo jambo lolote ni lazima viongozi wa Serikali mbili washauriane. Mambo haya si ya kulazimisha...,” alisema.
Uongozi wa Magufuli
Rais huyo alisema anamfahamu Rais Magufuli tangu akiwa waziri na anajua uwezo wake, “Majipu anayoyatumbua Rais habahatishi kwani anafanya vile kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, na si kwamba mimi situmbui, natumbua sana, sema mimi staili yangu siyo ya kusema kila kitu na waandishi wa huku (Zanzibar) si wafuatiliaji sana kama wa Bara,” alisema Dk Shein.
Aliongeza kuwa watu hawawezi kujua utumbuaji wake kama waandishi wa habari si wafuatiliaji, vilevile hawezi kuyajua majipu zaidi kama waandishi wa habari hawajayaibua, “Waandishi wa habari wa Zanzibar ni tofauti sana na wa Bara.”
Akizungumzia kauli ya Rais Magufuli kuwa awe mkali, Dk Shein alisema, “Kwa kuzungumza mimi ni mpole lakini mtu akikosea, mimi ni mkali kwelikweli, sema mimi siyo mtu wa kukasirika ovyo, busara zinaniongoza sana, japokuwa ukikosea sikuachi hata kidogo,” alisema Dk Shein.
Alisema katika kipindi chote ambacho amekaa madarakani, anajivunia kuifanyia Zanzibar mambo mengi na bado anaendelea.
“Katika utawala wangu nimeanzisha mpango wa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, sasa wazazi wanachangia ada ya mitihani tu ya kidato cha nne na cha sita na yenyewe muda si mrefu nitaiondoa,” alisema Dk Shein.
Kuhusu afya, alisema licha ya Wazanzibari wengi kutibiwa nje ya visiwa hivyo kwa madai ya kukosekana kwa huduma bora, Serikali yake imeongeza vituo vya afya kutoka 31 hadi 154, ingawa bado kuna changamoto ya wataalamu.
Dk Shein aligusia suala la mrithi wake akisema yeyote atakayeonesha nia kupitia CCM kwa wakati huu, atakuwa anakosea licha ya kwamba huu ndiyo muhula wake wa mwisho.
“Hata kama namfahamu mtu ambaye naona anafaa, siwezi hata kumnong’oneza mpaka pale atakapopitishwa na chama,” alisema Dk Shein
|
Navigation
Post A Comment: