Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa waandishi wa habari nchini kuandika
habari zinazohamasisha maendeleo ya nchi badala ya kuandika habari ambazo
hazina manufaa kwa taifa.
Akizungumza wakati ya hafla ya
kuwaapisha mawaziri, mabalozi pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu jijini
Dar es Salaam leo, Rais Magufuli alisema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa
kuwa wazalendo kwa kuandika habari za kuhamasisha wananchi kushiriki katika
shughuli za maendeleo pamoja na kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali.
“Nchi yetu ina sifa nzuri nje,
Rais wa Benki ya Dunia alipotembelea katika nchi yetu hivi karibuni
alitupatia jumla ya shilingi trilioni 1.74 na benki hiyo ipo mbioni
kutupatia fedha nyingine shilingi trilioni 2.8, lakini vyombo vyetu vya habari
haviandiki kwa mapani juu ya taarifa ” alisema Rais Magufuli.
Alibainisha kuwa fedha hizo
zitatumika katika miradi ya Ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo, maboresho
ya miji, pamoja na Vyuo Vikuu vya Sokoine na Mandela na kuleta
maendeleo ya nchi yetu lakini taarifa zake hazikupewa uzito unaostahiki katika
vyombo vya habari.
Rais Magufuli aliwataka
wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari kufuata uweledi wa
taaluma ya habari pamoja na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya
mtu mmoja mmoja.
Aidha, Rais Magufuli
amewapongeza viongozi aliowaapisha na kuwataka kufanyakazi kwa bidii na
juhudi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa
kutekeleza agenda ya viwanda.
Viongozi walioapishwa ni Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa
Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,
Alfayo Kidata.
Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Israel Job Masima, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Sylvester Mabumba pamoja na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Stellah Mugasha.
Na. Immaculate Makilika-
MAELEZO
Post A Comment: