Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita akizungumza wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mkoani humo kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo.
Wito
umetolewa kwa wafanyabiashara na wananchi wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi
katika Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa ajili ya kuwasilisha
malalamiko, changamoto, maoni pamoja na kupata elimu ya masuala ya kodi na
ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ujumla.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mhandisi Robert
Gabriel amesema kuwa, wafanyabishara na
wananchi watumie fursa ya kampeni hiyo itakayomalizika tarehe 13 Aprili, 2018
kupata elimu sahihi ya masuala ya kodi na tozo mbalimbali.
“Nachukua
fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote wa mkoa huu hususani
wale wanaoishi katika maeneo ya Masumbwe, Ushirombo, Rulembela, Katoro,
Lunzewe, Namonge, Nyanghw’ale, Bwanga na Muganza kujitokeza kwa wingi ili
waweze kujifunza, kupata huduma na kutoa maoni yao kwa watalaam wetu wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kuyatolea ufafanuzi na kuyafanyia kazi,”
amesema Mhe. Luhumbi.
Nae
Meneja wa TRA mkoani hapa, James Jilala amesema kuwa, lengo kuu la kufanya
kampeni hii maalumu ni kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na
kupokea mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa
ujumla.
“Kampeni
hii ni mwendelezo wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi iliyofanyika nchi nzima
kuanzia tarehe 5 hadi 9 Machi, 2018 katika ngazi ya mkoa. Kutokana na matokeo
ya kampeni ile mkoani hapa, tumeona ni muhimu tuwe na kampeni nyingine maalumu
ambayo inafanyika maeneo mbalimbali katika wilaya zetu tofauti na ile ya kwanza
iliyofanyika Geita mjini tu,” amefafanua Jilala.
Kwa
upande wake kiongozi wa timu ya watalaam kutoka TRA Makao Makuu Maternus Mallya
ameeleza kuwa, timu yake imejipanga vizuri na tayari kazi imeanza kufanyika
katika vituo vyote vilivyotengwa kwa ajili ya kampeni hiyo.
“Hapa
ninapozungumza, wenzangu wako kwenye maeneo husika wanaendelea kufanya kazi.
Hivyo, kama alivyosema Mhe. Mkuu wa Mkoa, nami natoa rai kwa wananchi wote
mkoani hapa, kujitokeza kwa wingi ili waweze kukutana na watalaam wetu kwa
ajili ya kupata huduma na elimu ya mlipakodi,” amesema Mallya.
Kampeni
Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani Geita imeanza leo tarehe 9 hadi
13 Aprili, 2018 ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara na wananchi
watasajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na
kuelimishwa kuhusu ulipaji wa Kodi ya Majengo kwa njia ya kieletroniki.
Post A Comment: