Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi na Viongozi Mkoani
humo kutoa ushirikiano kwa wadadisi na wataalam wa Takwimu katika utafiti wa
mapato na matumizi ya kaya binafsi unaoendelea hapa nchini ili kuwezesha
upatikanaji wa takwimu halisi na sahihi
Mkoani humo.
Mtaka
ameyasema hayo katika Mkutano wake na waandishi wa habari, wataalam wa Takwimu na
Viongozi wa madhehebu ya dini uliofanyika Februari 28 Mjini Bariadi.
Amesema Utafiti huo utatoa
makadirio ya uchumi jumla(macroeconomic), hususani matumizi ya kaya kwa ajili ya
Pato la Taifa (Gross Domestic Product-GDP), kupata mwenendo wa matumizi ya moja
kwa moja ya kaya ili kuwezesha uchambuzi
wa hali ya soko na kupata taarifa za umilikaji wa vifaa vya kudumu pamoja na
nyenzo za uzalishaji wa kipato.
Amesema kwa mujibu wa sheria
namba 9 ya mwaka 2015 kila mwananchi anawajibika kushiriki katika utafiti kwa
kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu rasmi
ambazo zitatumika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.
“ Lengo mama la utafiti huu ni
kujua hali ya kipato kwa kaya zetu asije mtu akapotosha kuwa watafiti wana agenda
nyingine, ndiyo maana nimeona viongozi wa Dini nao walifahamu hili ili wasaidie
kuwaeleza kwa ufasaha waumini wao; Serikali inahitaji takwimu sahihi ili ipange
bajeti na kuweka mipango ya maendeleo, niwaombe
wananchi na viongozi tutoe ushirikiano” alisema
Mtaka.
Aidha, amemuagiza Meneja wa
Takwimu mkoani humo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ushiriki wao katika
utafiti huu hususani kaya zilizochaguliwa na akamtaka yeye na wataalam wa
Takwimu wa Mkoa huo kufanya mikutano katika minada na magulio pamoja na maeneo
ya yenye idadi kubwa ya watu yakiwemo ya Makao Makuu ya Wilaya na miji
midogo(centers) ili kujenga uelewa kwa wananchi.
Meneja wa Takwimu Mkoa wa Simiyu,
Nestory Mazinza amesema tangu utafiti huu uanzae Desemba Mosi 2017 jumla ya
kaya 102 zimeshafanyiwa utafiti kati ya 408 zinazotarajiwa kufikiwa mpaka kumalizika
kwa zoezi hilo mwezi Novemba 2018.
Naye Bi.Joyce Luhende Mdadisi
kutoka Wilaya ya Meatu amesema wanapofanya utafiti huu wanakutana na changamoto
mbalimbali na kubwa ikiwa ni baadhi ya wanakaya kuogopa kutoa taarifa
zinazohitajika wakati wakihojiwa hali inayopelekea kukosekana kwa taarifa
sahihi.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi
wa Dini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikiristo Tanzania(CCT) Mkoa wa Simiyu,
Mchungaji Martine Samson Nketo amesema kupitia ibada watasaidia kuwahamasisha wananchi kushiriki
katika utafiti huu na kuwaeleza umuhimu wake katika mipango ya maendeleo
inayopangwa na Serikali.
Kaya zilizochaguliwa k kufanyiwa utafiti huu zinatoka katika maeneo 34 (Vijiji/Mitaa)
kwenye Wilaya zote tano za Mkoa wa Simiyu yaliyopo katika kata za Nkindwabiye,
Nyangokolwa, Sakwe, Nyakabindi, Dutwa, Matongo,Gilya, Sima,Mwamtani, Mwaswale,
Mwamapalala, Nhobora, Zagayu, Kinang’eli, Mwanhuzi, Mwandoya, Sakasaka,
Mwabuma, Lubiga, Ng’oboko, Busilili, Seng’wa, Masela, Mwamashimba, Buchambi,
Badi, Nyalikungu, Kiloleli,Kalemela, Mkula na Ngasamo.
Post A Comment: