WIZARA YATOA RAMBIRAMBI VIFO VYA WATOTO WATATU MKOANI GEITA

Share it:

Image result for Ngao ya Taifa

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
WIZARA YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA VIFO VYA WATOTO WATATU WALIOKUFA MAJI MKOANI GEITA
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imepokea kwa huzuni na simanzi kubwa tukio la watoto 24 wanafunzi wa shule ya msingi kuzama majini na watatu kati yao kufa maji wakati wakitoka shuleni katika Kijiji cha Butwa, wakielekea nyumbani Kitongoji cha Lulegea, Kata ya Izumacheli wilayani Geita.
Ajali iliyotokea na kusababisha vifo vya watoto watatu ambao ni Kumbuka Bruno Thomas (13) mwanafunzi wa darasa la tano, Anastazia Christopher (12) darasa la tatu na Sophia Muungano (11) darasa la pili; “imetupa huzuni kubwa kwani imetokea wakati watoto hao wakirejea nyumbani katika jitihada za kupata haki ya elimu katika kuwaandaa kuwa na maadili mema, stadi, na maarifa ya kutumikia taifa na familia kwa ujumla.
Katika kuepusha kadhia hii, Wizara inaunga mkono agizo la Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhakikisha kuwa inashirikiana na wananchi kujenga shule kwenye kisiwa cha Lulegea ili kupunguza safari za majini ambazo kwa kiasi kikubwa ni hatarishi kwa usalama, ulinzi na uhai wa watoto wetu.  
Wizara inatoa pole kwa wazazi, walezi, na marafiki wa watoto waliopoteza maisha, Tunaomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwa kuondokewa na watoto hawa ambao walikuwa wanaandaliwa kuwa nguzo na tegemeo kwa familia na Taifa.
Erasto T. Ching’oro
K.n. y: Kaimu Katibu Mkuu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
24/05/2017
Share it:

habari

Post A Comment: