ZANZIBAR YAPIGA HODI FIFA, WANAMICHEZO WAOMBWA KUZIDI KUOMBA DUA

Share it:





Hivi karibuni Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limeendelea na jitihada zake za kuhakikisha Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) wanapata uanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) baada ya TFF kuiombea ZFA kuwa Mwanachama wa Shirikisho hilo.

Kamati Tendaji ya Chama cha mpira wa miguu Zanzibar ZFA imekutana juzi  na Wenyeviti na Makatibu wa ZFA wilaya saba za Unguja chini rais Ravia Idarous Faina kwenye ukumbi wa uwanja wa Amaan.

Wajumbe wa kikao hicho kilichoitishwa na kiongozi huyo wa juu wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar waliweza kupokea taarifa mbili muhimu kutoka kwa rais huyo.

Katika hatua ya kwanza rais Ravia amewasilisha barua iliyotumwa na TFF kwenda Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA kuhusiana na maombi ya ZFA ambapo Wajumbe hao walipokea kwa furaha taarifa hiyo.

TFF tayari imeshatuma Barua rasmi FIFA kuhusu suala hilo lilalosubiriwa kwa hamu na wapenda soka wa Visiwa vya Zanzibar kuwa na uwezo wa kushiriki moja kwa moja michezo ya Kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho hilo la Dunia ikiwemo Kombe la Dunia.

Afisa habari wa ZFA Ali Bakar “Cheupe” amesema Wajumbe wa ZFA wamepokea kwa furaha kubwa taarifa ya maombi hayo ambapo amewataka Wazanzibar kuzidi kuomba dua ili Zanzibar ipate uanachama kamili wa FIFA.

“Wanzibar nawaomba tuzidi kuomba dua ili tufanikiwe kupata uanachama wa FIFA, kama walivyoomba tukapata CAF basi tuwe pamoja kwa hili pia”.

Zanzibar iliingia katika kitabu cha historia Siku ya Alhamis Machi 16, 2017 baada ya ZFA kuingizwa rasmi kuwa Mwanachama wa 55 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF” kufuatia Kikao cha 39 cha Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo kilichofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia.

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.



Share it:

michezo

Post A Comment: