WANANCHI WASHIRIKI KUCHIMBA MTARO WAPATE MAJI.

Share it:
Wananchi wa kijiji cha Busese kata ya Kasoli wakichimba Mtaro iliwaweze kuwekewa mabomba kuelekea kwenye makazi yao ambapo mradi huo umefadhiliwa na kampuni ya Kuchambu pamba ya Alliance Ginnery iliyoko Kasoli wilayani bariadi mkoani Simiyu.
Diwani wa kata ya Kasoli Mayala Shiminji (mwenye shati la drafti mikoni mirefu) akishiriki na wananchi kuchimba Mtaro ili waweze kuwekewa mabomba kuelekea kwenye makazi yao ambapo mradi huo umefadhiliwa na kampuni ya Kuchambu pamba ya Alliance Ginnery iliyoko Kasoli wilayani bariadi mkoani Simiyu.


IMEANDALIWA NA  COSTANTINE MATHIAS (BARIADI).

Wananchi wa kijiji cha Busese kata ya Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu wamechangia nguvu zao katika kuchimba mtaro kwa ajili ya kutandaza mabomba ya maji ili waweze kupata huduma hiyo katika maeneo yao ambapo mradi huo umetolewa na Kampuni ya Kuchambua Pamba ya Alliance Ginnery .

Akiongea wakati zoezi la uchimbaji likiendelea mtendaji wa kijiji hicho Abdallah Mustapha alisema kuwa awali kulingana na maelekezo ya mwekezaji wananchi wangeyapata maji katika chanzo chake umbali wa kilomita moja lakini kwa sasa yatavutwa kuwafikia wananchi.

Alisema kuwa wananchi walikuwa na changamoto kubwa ya maji hivyo walilazimika kutumia maji ya kutoka kwenye madimbwi ambayo hayakuwa safi na salama hata kwa matumizi ya mifugo.

‘’visima vilivyokuwepo havikidhi mahitaji ambapo tulikuwa tunauziwa ndoo ya maji ya lita 20 kwa silingi 300 wakati ni kijijini, hivyo baada ya mradi huu tulikaa na kupendekeza maji yasogezwe kwa wananchi ndiyo maana sasa wananchi wenyewe wameshiriki uchimbaji wa mitaro ya kutandaza mabomba kwenda katika maeneno yao’’ alisema Mustapha.

Aliongeza kuwa mara baada ya mradi kuanza kutoa maji wamekubaliana ndoo moja itauzwa kati ya shilingi 20 hadi 30 na fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuajiri mlinzi, ukarabati wa vifaa na kuyatibu maji pindi wanapohisi yamechafuka.

Aidha Mtendaji huyo aliitaka serikali kuunga mkono juhudi za Mwekezaji huyo pamoja na wananchi kwa kuwaongezea huduma ya maji kwa sababu hitaji la maji haliwezi kutosha kutokana na matumizi yake kuwa mengi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Mayala Shiminji alisema kuwa mmradi huo wa visima virefu unatekelezwa na mwekezaji huyo katika vijiji vitatu vya Busese, Nduha na Mwamlapa.

Alisema kuwa kulingana na tahimini ya wataalamu wa maji mradi huo kwa sasa unaweza kutoa lita 4000 kwa saa moja hivyo utaweza kukidhi mahitaji ya wananchi zaidi ya 600 katika eneo hilo la Busese.

Aliongeza kuwa katika maeneo mengine ya kata yake serikali imeshatoa maelekezo na mpango wa kuyatoa maji kwenye chanzo na kuyapeleka katika maeneo ya wananchi walipo kwa kutumia umeme wa jua (sola).

Baadhi ya wananchi walioshiriki katika uchimbaji huo wamempongeza mwekezaji huyo wa kiwanda cha pamba kwa kuwachimbia kisima cha maji ambacho kitatatua kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

‘’awali maji yalikuwa ya shida sana kwetu wakazi wa eneno hili…baada ya mradi huu tumejumuika ili na sisi kuchangia nguvu zetuu kwa kuchimba mtaro ili maji yaweze kutufikia katika maeneo yetu’’ alisema Grace Samsoni.

Naye Anastazia Joseph anasema kuwa awali maji walikuwa wakiyapata kwa taabu sana hasa maeneno ya milimani ambapo walikuwa wakishambuliwa na wanyama pia walikuwa na hofu ya kutembea usiku kutafuta  maji.

Meneja wa kiwanda cha kuchambua Pamba cha Kasoli Boaz Ogolla alisema kuwa kwa kushirikiana na wananchi wametoa huduma hiyo ili kuweza kuwatatulia kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji.

Ogola alisema kuwa katika mradi hiyo pamoja na mingine vitachimbwa katika kata hiyo ambapo visima vitano vitaghalimu kiasi cha milioni 200 lengo likiwa ni kusogeza huduma za kijamii .

“katika bajeti yetu tutenga milioni 200 kwa ajili ya kuchimba visima virefu katika kata hiyo na wananchi tumeshawashirikisha na wameitikia kwani visima hivyo vitasaidia jamii kufanya shughuli za kimaendeleo kwa kiasi kikubwa tofauti na sasa hasa wakinamama muda mwingi wanahangaika kuchota maji”alisema Ogola.

Alibainisha kuwa wao kama wawekezaji watahakikisha jamii wanayoishi nayo wanaisaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwani bila wananchi kujishughulisha hata uwepo wa kiwanda hicho ni sawa na bure na kwamba hakiwezi kufanya shughuli ya uzalishaji.

Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance kwa mwaka huajiri watu zaidi 500 huku suala la uboreshaji wa huduma za jamii na miundombinu yake linapewa kipaumbele ili wananchi wa eneo husika waweze kunufaika na uwekezaji huo, huku wazawa wakipewa kipaumbele katika ajira.


Share it:

habari

Post A Comment: