Na Fatma Salum – MAELEZO
Tume ya Kudhibiti UKIMWI
Tanzania (TACAIDS) imeendelea kuiasa jamii kuhusu kubadili tabia ili kuepuka
maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani ugonjwa huo bado ni janga kwenye nchi
yetu.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa tume hiyo Bw.Jumanne Issango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio na changamoto za tume tangu ilipoanza
kutekeleza majukumu yake.
“UKIMWI bado ni changamoto
katika maendeleo ya Taifa letu na umeendelea kuathiri kila sekta, kila imani,
matajiri na masikini nchini kote hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujitathmini
mwenendo wake na kuacha tabia hatarishi ambazo zinachangia kuongeza maambukizi
ikiwemo uasherati, ngono zembe, ulevi na kadhalika,” alisema Issango.
Alieleza kuwa kwa miaka ya
karibuni hali ya maambukizi ya UKIMWI imeendelea kupungua ingawa kuna tofauti
kwenye mikoa, wilaya na makundi ya kijamii.
Issango alibainisha kuwa
kiwango cha maambukizi Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na takwimu hizo ni
kutokana na Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI mwaka 2012.
Kwa mujibu wa utafiti huo
wanawake walioambukizwa ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8 ambapo idadi
ya Watanzania wanaokadiriwa kuishi na VVU ni zaidi ya milioni 1.5.
“Mikoa inayoongoza kuwa na
maambukizi makubwa ni Njombe asilimia 14.8, Mbeya asilimia 9 na mikoa yenye
maambukizi ya chini zaidi ni Manyara asilimia 1.5, Tanga asilimia 2.4 na Dodoma
asilimia 2.9,” alifafanua Issango.
Aidha alisema kuwa licha ya
maambukizi mapya kupungua kwenye jamii bado kiwango cha maambukizi kwenye makundi
maalum kimeendelea kuongezeka.
Akitaja makundi hayo Issango
alisema kuwa ni pamoja na madereva wa magari ya masafa marefu, wachimba madini,
wavuvi, wafungwa na wale wanaofanya biashara ya ngono.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Muitikio wa Kitaifa kutoka Tume hiyo Bi. Audrey Njelekela
alisema Serikali kupitia TACAIDS inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana
na janga hilo ikiwemo kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti itakayosaidia
kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
“Mkakati wa Tatu wa Taifa wa
Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18 unalenga ifikapo 2018 kiwango cha maambukizi
kishuke kufikia asilimia 0.16 ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo utafiti unaonesha
maambukizi ni asilimia 0.32,” alisema Njelekela.
Alitaja hatua nyingine
zinazochukuliwa na tume hiyo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma hasa
kwa vijana, wanawake wajawazito na makundi maalum ikiwemo kujenga Vituo vya
Maarifa vinavyotoa huduma za VVU/UKIMWI kwa madereva wa magari ya masafa
marefu.
Aliongeza kuwa juhudu za
Serikali kutoa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zimesaidia
kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ambapo kwa sasa wanaotumia dawa hizo
ni zaidi ya watu laki 8.
Pia Serikali imeanzisha Mfuko
wa Udhamini wa Shughuli za Kudhibiti UKIMWI kwa ajili ya kusaidia kununua dawa,
kutoa elimu ya UKIMWI, kupima, kufanya tafiti na kutoa elimu ya uzazi kwa
vijana.
TACAIDS ilianzishwa kwa
Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 2001 kwa lengo la kutoa uongozi wa kimkakati,
uratibu na kuimarisha juhudi za wadau wote wanaojishughulisha na kudhibiti
UKIMWI nchini.
Post A Comment: