Mkurugenzi wa
Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginnery, Ndg. Boazi Ogola(wa pili
kushoto) akimuongoza Waziri wa Kilimo, Dkt.Charles Tizeba (aliyeweka mkono
kifuani) na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Bariadi na Mkoa wa Simiyu kuelekea
kuona kiwanda hicho wakati wa ziara ya Waziri huyo Mkoani Simiyu.
Na
Stella Kalinga, Simiyu
Waziri wa Kilimo Mhe.Dkt. Charles Tizeba amewataka
wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba(jineri) kupeleka pamba mbegu kwenye
kiwanda cha kuchakata(kutoa manyoya) mbegu za pamba cha Quton na akasema
watakaogoma kupeleka hawatanunua pamba msimu ujao.
Waziri Tizeba ameyasema hayo jana alipotembelea
kiwanda hicho katika Kata ya Kasoli wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwa lengo
la kujionea hali ya uzalishaji wa mbegu ya pamba inavyoendelea.
Amesema suala la wenye viwanda vya kuchambua
pamba(ginners) kupeleka pamba mbegu katika kiwanda cha kuchakata mbegu za pamba(kuondoa
manyoya) siyo la hiari na walishapewa maelekezo, hivyo wanapaswa kupeleka pamba
mbegu katika kiwanda cha Quton ili zitolewe manyoya na baadaye zipelekwe kwa
wananchi.
“ Nimeambiwa watu wa Quton wanashindwa kufanya kazi
kwa shift tatu kwa siku kwa sababu walio na mbegu kwenye viwanda vyao vya
kuchambua pamba hawataki kuleta pamba hapa, wakati wanayo maelekezo na hii siyo
hiari mbegu ikishatengwa na Bodi ya Pamba si yao” alisema Tizeba.
“Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nakuagiza wapelekee
ujumbe huu kwamba ginner atakayegoma kuleta pamba mbegu hapa Quton hanunui
pamba mwaka kesho, wanapaswa walete mbegu zitolewe manyoya ziende kwa wananchi ili
wapate mbegu bora, katika hili sitabembelezana na mtu” alisisitiza Tizeba.
Aidha, Mhe.Waziri amesema mahitaji ya mbegu ya pamba
iliyotolewa manyoya kwa nchi nzima ni takribani tani 8000, hivyo ili kufikia
kiwango hicho katika siku zilizobaki kuelekea msimu wa kilimo cha pamba,
kiwanda cha Quton kinapaswa kufanya kazi saa 24 kwa kuwa uzalishaji wa sasa wa
tani 60 hadi 65 kwa saa 16 kwa siku hautaweza kufikia lengo hilo.
Wakati huo huo Waziri Tizeba ametoa wito kwa
wananchi Mkoani Simiyu kutopanda pamba sasa kwa kuhofia mvua kukatika mapema,
badala yake wasubiri taarifa rasmi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa juu ya hali ya
mvua katika ukanda huo itakayotolewa muda mfupi ujao,ambayo baadaye itatumika
kuwashauri wakati muafaka wa kupanda, japo alieleza kuwa taarifa ya jumla ya
utabiri wa hali ya hewa inaonesha mvua itanyesha juu ya wastani.
Pia Mhe.Waziri amewahakikishia wananchi kuwa bei ya
mbolea imeshuka, hivyo akawataka wataalam wa Kilimo kuwaelimisha wananchi juu
ya bei elekezi ya mbolea kwa kila wilaya, ili wasiuziwe kwa bei kubwa na
akasisitiza kuwa bei ya mbolea na mbegu mwaka 2018 itapungua zaidi kwa kuwa
Serikali imefuta takribani kodi 80 katika kilimo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo
Kiswaga amesema Mkoa wa Simiyu unazalisha pamba kwa wingi, ambapo katika msimu
wa mwaka 2016/2017 umezalisha takribani asilimia 65 ya pamba ya nchi nzima, hivyo akaomba
wananchi wa mkoa huo wasaidiwe kupewa mikopo ya zana bora za kilimo na pembejeo
nyingine kupitia mfuko wa pembejeo ili kuongeza uzalishaji zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Quton Tanzania Limited
Ndg. Pradyumansinh Chauhan amemuomba Waziri wa Kilimo kuhamasisha wananchi
kutumia mbegu za pamba zilizotolewa manyoya ili kuongeza uzalishaji kwa kuwa
hazishambuliwi kwa urahisi na magonjwa na zinapunguza kiasi cha mbegu kinachotumika
shambani ambapo kilogramu sita tu hutumika kwa hekali wakati zenye manyoya hutumika
hadi kilogramu 15.
|
Post A Comment: