Jonas
Kamaleki - MAELEZO
Ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 40
katika kipindi cha Julai- Septemba 2017 ikilinganishwa na kipindi hicho hicho
mwaka jana.
Hayo yameelezwa leo katika mahojiano maalum kati Mwanasheria
wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Deus Sokoni na
Idara ya Habari (MAELEZO).
Sokoni amesema katika kipindi cha Julai – Septemba mwaka
2016 ajali za barabarani zilikuwa 2639 wakati mwaka huu katika kipindi hicho
hicho jumla ya ajali 1375 zimetokea nchini.
Kwa mujibu wa Kamanda Sokoni, idadi ya vifo pia
imepungua kutoka 923 hadi 652 na ajali za pikipiki zimepungua kutoka 653 hadi
367 ambayo ni sawa na asilimia 44.
“Kupungua kwa ajali hizo na vifo imetokana na
madereva kutii sheria bila shuruti, ushirikiano baina ya wananchi na jeshi la
polisi na elimu kwa umma ambayo tumekuwatukiitoa kwa wadau mbalimbali, ikiwemo
wanafunzi, vituo vya bodaboda na kambi za jeshi la wananchi,” alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni amesema makosa yanayotokana na ulevi
yameongezeka kutoka 7589 hadi 7617 jambo ambalo limeelezwa kuwa elimu bado
inahitajika ili kupunguza changamoto hiyo.
Majeruhi wa ajali za barabarani wamepungua kutoka
570 hadi 284 ambayo ni sawa na takriban asilimia 50 jambo ambalo linaonyesha
mabadiliko makubwa katika kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Sokoni aliongeza kuwa elimu inayotolewa kwa
waendesha pikipiki imesaidia kupunguza ajali na vifo vya waendesha pikipiki na
abiria kiasi kwamba kwa mwaka 2016 katika kipindi husika vifo vilikuwa 246 na
kwa mwaka huu ni 182.
Kupungua kwa ajali, majeruhi na vifo kumetokana na Mkakati
wa Kitaifa chini ya Kikosi cha Usalama Barabarani wa kupunguza ajali za
barabarani zinasosababisha majeruhi na vifo.
Kamanda Sokoni amewataka madereva, watembea kwa
miguu, abiria na wadau wote wa usafiri kuzingatia sheria kanununi na taratibu
za usalama barabarani.
Katika kutekeleza Mkakati huo zimefanyika operesheni
za usalama barabarani katika mikoa ya Njombe, Tanga, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha
na Manyara. Katika operesheni hizo madereva 64 wamefungiwa leseni, wengi wao
wakiwa madereva wa mabasi ya abiria ambapo madereva 14 wamefungwa jela.
Usalama barabarani ni jukumu la kila mtu, kwani
watanzania karibu wote ni watumia barabara, hivyo kila mmoja inabidi awe
mwangalifu katika sula hilo.
Ikumbukwe Kauli Mbiu ya Wiki ya Nenda kwa Usalama
Barabarani ya mwaka huu ilisema Zuia ajali, Tii Sheria, Okoa Maisha. Hivyo,
madereva na waenda kwa miguu pamoja na abiria inabidi watii sheria bila shuruti
ili kuzuia ajali na kuokoa maisha.
Post A Comment: