NA
COSTANTINE MATHIAS, MASWA.
MAHAKAMA ya wilaya ya Maswa mkoani
Simiyu imemhukumu Mwenyekiti wa Baraza la ardhi na Nyumba katika wilaya hiyo, Mdimi
Ilanga kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh Milioni 1.4 baada ya
kupatikana na hatia na makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu
Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Fredrick Lukuna alisema kuwa ameridhika
na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka.
Alisema kuwa anamtia hatia
mshitakiwa baada ya kujiridhisha kupitia mashahidi walioletwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuthibitisha kuwa alitenda makosa hayo
ya kuomba na kupokea rushwa kiasi cha Sh 400,000 kutoka kwa Paul Shigela.
Kabla ya hukumu hiyo Mwendesha
mashitaka wa Takukuru,Mzalendo Widege aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali
kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa serikali waliopewa
dhamana ya kusimamia haki kujiingiza katika vitendo vya kuomba na kupokea
rushwa kwa lengo la kupindisha haki.
Ilidaiwa mahakamani hapo na
Mwendesha mashitaka wa Takukuru,Widege kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo
kutoka kwa Paul Shigela ambaye alikuwa na shauri la madai Namba 103
la Mwaka 2016 katika baraza hilo.
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo
kuwa mtuhumiwa aliomba kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Shigela ili aweze
kumpatia upendeleo wa maamuzi katika shauri lake hilo lililokuwa mbele yake.
Alizidi kuieleza mahakama hiyo kuwa
mshitakiwa alitenda makosa hayo mawili januari 27 mwaka huu ndani ya
ofisi ya baraza hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kwa kosa la kuomba rushwa na
Kifungu cha 15 (1) (a) Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya
mwaka 2007 kwa kosa la kupokea rushwa .
Katika kesi hiyo Na 14 ya
Mwaka 2017 mara ya kwanza baada ya mshitakiwa kusomewa shitaka hilo
alikana kosa linalomkabili na kuiomba mahakama kufuta kesi inayomkabili kwa
kile alichoeleza kuwa kukiukwa kwa kanuni za kukamatwa na kuwekwa
mahabusu jambo ambalo mahakama halikulikubali.
|
Navigation
Post A Comment: