Mkuu wa Mkoa wa Geita Robert Gabriel akihutubia wananchi(awapo katika Picha) wakati wa wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama barabarani Mkoani Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amemuagiza Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa
Geita Alfred Hussein kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria
waendesha pikipiki wote wasiovaa kofia ngumu maarufu kama element wanapotimiza
majukumu yao ya usafirishaji wa abiria.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama
barabarani ambayo kimkoa yanafanyika Mji mdogo wa Katoro Wilaya ya Geita Mheshimiwa
Robert Gabriel amesema muendesha piki piki yeyeto asiyevaa kofia ngumu Mkoani
humu akamatwe na kuwekwa ndani ili liwe
fundisho kwa watu wote wasiopenda kutii sheria na matokeo yake wanasababisha
vifo kwa jamii.
"Naamini kuanzia wakati huu RTO na Kamati za Usalama
barabarani Mkoa na Wilaya mtu asiyevaa kofia ngumu atakamatwa na kuwekwa ndani
tutatumia sheria zote hakuna kupatana hakuna kuelewana". Ameongeza kuwa
watumiaji wa vyombo vya moto wanatakiwa kuelimishwa na kufundishwa taratibu zinazowaongoza
katika utumiaji wa vyombo hivyo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
pamoja na vyombo vyao wapate elimu ili kujua mbinu za kuwafanya kuwa salama.
Mhandisi Robert Gabriel amewataka abiria kutoa taarifa kwa vyombo vya
usalama pamoja na kutowaruhusu madereva kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo
kasi kwa kuwa jukumu la Usalama ni la kila mwananchi.
Aidha, amekipongeza kikosi cha usalama barabarani mkoani hapa kwa kazi
nzuri ya kuzingatia usalama wa wananchi katika barabara, amewataka waendelee kusimamia suala hili na
kuchukua hatua pale inapobidi.
Awali Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoani hapa ndugu Alfred
Hussein alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kuwa ajali za barabarani zimepungua kutoka
ajali 87 mwaka 2016 hadi kufikia ajali 68 kwa mwaka huu. Vile vile ameeleza
kuwa idadi ya vifo pia imepungua kutoka vifo 98 mwaka 2016 hadi vifo 79 kwa
mwaka huu wa 2017.
Alfred ameongeza kuwa kwa ajali
nyingi zinasababishwa madereva kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia
vilevi mbalimbali, mwendo kasi, kukosa umakini barabarani, uchakavu wa vyombo
vya usafiri na miundombinu. Maadhimisho
haya yanafanyika kwa wiki nzima ambapo wananchi, madereva na wamiliki wa vyombo
vya moto wanapata elimu kwa lengo la kuhakikisha kila mtu anajikinga na ajali
za barabarani.
|
Post A Comment: