Baadhi ya
Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Simiyu wakifuatilia hoja mbalimbali
zilizokuwa zikiwasilishwa katika Kikao Bodi hiyo kilichofanyika Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa Wakala wa Barabara Mijini na
Vijijini(TARURA) Mkoani humo kusimamia utekelezaji wa Miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja kwa kuzingatia
weledi.
Mtaka ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha Bodi ya
Barabara ya Mkoa huo, kilichofanyika jana Jumatatu Mjini Bariadi Mkoani humo.
" Nawaomba TARURA mfanye kazi kwa kuzingatia weledi,
siyo madaraja yanajengwa mnapeleka karavati zinavunjika kabla daraja
halijajengwa, mahali pa kuweka kokoto mnaweka udongo, mtaidhalilisha taaluma;
ningeomba mzingatie weledi kwa sababu mkifanya vibaya wananchi watatushtaki,watasema
tumeanzisha wakala ambaye hana maana kwao" amesema Mtaka.
Ameongeza kuwa Uongozi wa Mkoa wa Simiyu haujapata shida
juu ya miradi ya barabara inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Nchini
(TANROADS), hivyo ipo haja pia kwa TARURA kusimamia utekelezaji wa miradi yake
katika ubora, kwa kuwa Miradi hiyo imeondolewa katika Halmashauri (Mabaraza
ya Madiwani) na kupelekwa TARURA, ili ipangiwe mipango na kusimamiwa na
wataalam pekee kwa lengo la kuonesha utofauti kiutendaji na umuhimu wa
Wakala huo katika kuwapa huduma bora wananchi.
Wakati huo huo Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi Bilioni
86.1 kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara ya Bariadi -Maswa yenye urefu wa Kilomita
49.7 kwa kiwango cha lami, ambayo amesema ikikamilika itaifanya Bariadi na
Maeneo mengine ya Mkoa huo kama Malampaka(Maswa) kuwa maeneo ya kibiashara.
Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mji
Bariadi na Halmashauri ya Wilaya Maswa kutumia fursa hiyo kujenga vituo vya
mabasi vya kimkakati vitakavyoendana na kasi ya uingiaji wa magari mengi baada
ya kukamilika kwa barabara ya Maswa-Bariadi na Ujenzi wa Reli ya “Standard
Gauge” na Bandari kavu itakayojengwa
Malampaka wilayani Maswa.
Akiwasilisha taarifa ya barabara zinazosimamiwa na
TANROADS, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Albert Kent amesema
Barabara ya Bariadi-Maswa itajengwa kwa kutumia fedha za Serikali ya Tanzania
na itachukua muda wa miezi 24 mpaka kukamilika kwake, ambapo amebainisha kuwa
Mkandarasi Kampuni ya M/s CHICO ameshawasili eneo la kazi(site).
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.
Jumanne Sagini ameomba wazo la marekebisho ya Viwango vya fedha zinazotakiwa
kwenda TANROADS na TARURA ambalo lilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI, lifanyiwe kazi ili TARURA wapate fedha na kufanya kazi kwa weledi pamoja
na kusaidia barabara za Halmashauri zisife.
Sagini ameongeza kuwa Halmashauri zishirikiane na TARURA kutafuta
namna ya kuzifanyia matengenezo barabara za Vijiji ambazo haziko chini ya
usimamizi wa wakala huo (TARURA), lakini
ni za muhimu kwa maendeleo ya wananchi hususani zinazounganisha vijiji ili
kurahisisha mawasiliano kati ya kijiji na kijiji.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu,Mhandisi Peter Mosha
amesema mwaka 2017/2018 Mkoa huo umeidhinishiwa zaidi ya shilingi bilioni sita
kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye mtandao wa barabara wenye jumla ya
kilomita 1780.87 , madaraja na makaravati katika Halmashauri zote sita za
Mkoa
kulingana na mahitaji na mpango wa bajeti wa Halmashauri husika.
Naye Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Mhe. Mashimba
Ndaki amesema Wakala wa Barabara (TANROADS) unapaswa kuhakikisha barabara zote zinawekewa
vivuko ili kuwasaidia wananchi kuvuka kwa usalama.
Akipongeza kazi inayofanywa na TANROADS Mkoa wa Simiyu,
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga ameomba TANROADS kuona namna ya
kufanyia kazi kona nyingi zilizopo katika barabara ya
Bariadi-Lagangabili-Kisesa pamoja na kuangalia upanuzi wa barabara
mbalimbali zinazosimamiwa na Wakala huo ili zisisababishe uharibifu wa magari.
|
Post A Comment: