Mbunge
wa Itilima, Mhe.Njalu Silanga(kulia) akizungumza jambo wakati wa Ziara ya
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako (kushoto)
aliyoifanya wilayani Itilima.
|
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako akizungumza na
wananchi wa Kata ya Luguru wilayani Itilima (hawapo pichani) wakati wa Ziara
yake mkoani Simiyu.
|
Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako amesema Serikali inatarajia
kuanza ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) cha Mkoa wa Simiyu
kuanzia mwezi Machi, 2018.
Waziri
Ndalichako ameyasema hayo leo wakati
alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake ya
siku moja Mkoani humo.
“Kesho tarehe
28/12/2017 kwenye magazeti kutatoka tangazo la zabuni ya ujenzi wa VETA ya Mkoa
wa Simiyu na tunategemea kujenga VETA ya Kisasa itakayohudumia Mkoa na
inayoendana na mahitaji ya sasa; tukitangaza zabuni kesho itachukua siku 30
kupokea zabuni unahitajika mwezi mmoja kufanya tathmini, nawaahidi kuwa ujenzi utaanza
mwezi Machi” alifafanua Profesa Ndalichako.
Ameongeza kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inasisitiza juu ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda
inatambua umuhimu wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi ndiyo maana imejipanga
kujenga vyuo hivyo pamoja na kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Aidha, Profesa
Ndalichako amepongeza ongezeko la wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la
kwanza na akasisitiza kuwa Wizara ya Elimu ambayo ndiyo inayotunga Sera
itahakikisha inasimamia kikamilifu ili wanafunzi wote wanaoanza darasa la kwanza wamalize
masoma yao.
Amesema ongezeko
hilo ambalo limesababishwa na mwamko chanya wa wazazi baada ya kuanza
kutekelezwa kwa mpango wa elimu bila
malipo limepelekea upungufu wa miundombinu shule na ndiyo maana Serikali kuu inashirikiana
na Halmashauri pamoja na wananchi katika ujenzi wa miundombinu ili kukabiliana
na upungufu kupitia Mradi wa Lipa kulingana na Matokeo(P4R).
“Kupitia mradi
wa Lipa kulingana na Matokeo tumeshajenga jumla ya vyumba vya madarasa 1104,
matundu ya vyoo 3396, mabweni 261. Tunaendelea pia kuimarisha miundombinu
katika sekta ya elimu kwa ujumla, kwa maana ya ukarabati katika vyuo vya Ualimu
ambapo tumeshakarabati vyuo 17 na shule kongwe 46 kati ya shule 88
zimeshakarabatiwa” alisema Waziri.
Profesa Ndalichako
amepongeza Uongozi wa Wilaya ya Itilima kwa kutumia vizuri jumla ya shilingi
bilioni 2.177 za Mradi wa Lipa Kulingana na matokeo(P4R) ambazo zimetumka
kujenga miundombinu mbalimbali ya shule vikiwemo vyumba vya madarasa, mabweni
na matundu ya vyoo wilayani humo.
Akimshukuru
Waziri wa Elimu kwa kupeleka fedha za Mradi wa Lipa kulingana na matokeo (P4R)
katika Wilaya ya Itilima ambazo zimesaidia upatikanaji wa Mbunge wa Jimbo la
Itilima Mhe.Njalu Silanga amesema Wilaya hiyo imetekelezaji wa mradi huo kwa
kufuata taratibu na miongozo yote ya
Serikali kwa kushirikiana na wananchi.
Kwa upande wake
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema katika kipindi cha mwaka
2018-2020 Mkoa huo umejiwekea mpango wa kujenga mabweni kwa wanafunzi wa kike
katika kila shule ili kuwaondolea adha ya kutembea mwendo mrefu na changamoto
nyingine.
Hii ni ziara ya
kwanza kwa Waziri Ndalichako Mkoani Simiyu ambayo imempa nafasi ya kutembelea,
kuweka mawe ya msingi, kukagua na kufungua vyumba vya madarasa, mabweni katika
maeneo tofauti Wilayani Itilima ikiwemo Kijiji cha Habiya, Lagangabilili,
Itilima, Mahembe na baadaye kufanya mkutano wa hadhara katika kata ya Luguru.
Post A Comment: