Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa Simiyu
Halmashauri
ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeshauriwa kuwekeza katika kiwanda cha
kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo viatu, mikoba na
mikanda kinachomilikiwa na kikundi cha Usindikaji Ngozi Senani kilicho kata ya
Senani wilayani Maswa, ili kuongeza thamani ya ngozi zitokanazo
na mifugo.
Ushauri
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ziara
yake ya kutembelea viwanda vidogo katika wilaya MASWA.
Mtaka amesema katika
kutekeleza Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya Viwanda , Halmashauri
ya Maswa inapaswa kuwekeza katika viwanda vinavyoanzishwa na vikundi ili
kuviwezesha katika upatikanaji wa malighafi ya kutosha, kuongeza thamani ya
mazao ya mifugo pamoja na kilimo ili viwanda hivyo viweze kuzalisha kwa tija.
“Tungehitaji kuwa mkoa ambao
utawekeza sana katika viwanda vidogo na ndiyo maana tulianza dhana ya Wilaya
moja bidhaa moja kiwanda kimoja na sasa tunakwenda kwenye Kijiji Kimoja Bidhaa
Moja Kiwanda kimoja; tunataka kupunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje ya Mkoa”
alisema Mtaka.
Aidha, ameitaka Halmashauri
hiyo kuwasaidia wanakikundi kuweka mifumo mizuri ya kutengeneza soko la bidhaa
zinazozalishwa katika kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kuuza katika minada yote
ya wilaya hiyo na kuimarisha soko la nje.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt.Fredrick Sagamiko amesema
Halmashauri itahakikisha kiwanda hicho kinapata
malighafi ya kutosha ambapo amebainisha kuwa Halmashauri imeingia
mkataba na Chuo cha DIT Mwanza kuhakikisha kuwa inazalisha malighafi(ngozi) kwa
wakati kwa ajili ya kiwanda hicho.
Akiwa Malampaka ambapo
alitembelea Mradi wa Ghala na Mashine ya kukoboa mpunga na kupanga madaraja, Mtaka
amekipongeza Chama cha Ushirika Bumala AMCOS kwa kuanzisha kiwanda, huku
akiwataka wananchi wa eneo hilo kujiandaa
kiushindani katika biashara, kwa kuwa hivi karibuni Serikali inatarajia kuanza
ujenzi wa bandari ya nchi kavu itakayoenda sambamba na ujenzi wa Reli ya
Kisasa(Standard Gauge).
“Ni lazima mjiandae
kiushindani katika biashara, miaka mitatu ijayo katika Mipango ya Serikali
Malampaka haitakuwa kama ilivyo, hapa ni mahali ambapo Standard Gauge ikianza
bidhaa zitakuwa zikisafirishwa kwa wingi; nimeshaongea na Mkurugenzi kuwa eneo
hili lipimwe na Halmashauri imiliki eneo la uwekezaji” alisisitiza Mtaka.
Katika hatua nyingine Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka alitembelea eneo la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza ungalishe katika
Kijiji cha Njiapanda, ambacho kitamilikiwa na shule 30 za Halmashauri ya Wilaya
ya Maswa, kinachoanzishwa kwa lengo la kuongeza kipato cha shule na
halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na kuboresha lishe za watu.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Afisa Elimu Msingi
Wilaya ya Maswa, Mwl. Mabeyo Bujimu amesema shule za msingi 30 wilayani humo
zitanufaika kwa kulima viazi lishe na kukiuzia kiwanda hicho kama malighafi
pamoja na kuuza bidhaa zitakazozalishwa na kiwanda.
Huu ni mwanzo wa ziara ya
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ambayo amepanga kutembelea viwanda
vidogo vilivyopo katika wilaya zote za mkoa huo.
Post A Comment: