UCHUNGUZI WAANZA KUBAINI WALIOMUUA KWA RISASI MWANAFUNZI CHUO CHA USAFIRISHAJI

Share it:




*Wizara ya Mambo ya Ndani yaelezea kinachoendelea
*Rais Magufuli aagiza waliohusika wachukuliwe hatua 

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imewahakikishia Watanzania kuwa uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Aqwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi utafanyika kwa haraka na weledi mkubwa na kufafanua waliohusika na kifo hicho kwa namna yoyote ile hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Imesema tukio la mwanafunzi huyo limewasikitisha Watanzania wote na Wizara hiyo imeanza kufanya uchunguzi ili kupata taarifa sahihi za tukio la kupigwa risasi mwanafunzi huyo na kwamba iwe kwa ofisa wa polisi au viongozi wa kisiasa wakithibitika kuhusika watachukuliwa hatua ili iwe fundisho kwa wengine kwani Serikali haipo tayari kuona raia hata mmona anapoteza maisha.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Masaun Yusufu Masaun wakati anaelezea tukio la kifo  chwa mwanafunzi Aqwilina aliyekuwa anasoma mwaka wa kwanza katika chuo hicho.

UCHUNGUZI WAANZA 

Akizungumzia hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa kutokana na mauaji ya mwanafunzio huo, Masaun amesema tayari vyombo vya ulinzi na usalama vimenza kuchunguza tukio hilo ili kubaini waliohusika na kwa sasa ni mapema kusema fulani ndio amehusika moja kwa moja.

Amesema Serikali imesikitishwa na kifo hicho lakini uchunguzi unaendelea na atakayebainika kuhusika kwa namna yoyote hatua za kisheria zitachukuliwa.

"Tutahakikisha hatua zinachukuliwa haraka kwa waliohusika na hakuna ambaye ataachwa iwe ofisa wa polisi au viongozi wa vyama vya siasa.Kiujumla matatizo ya uvunjifu wa amani lazima yachukuliwe hatua na waliohusika kwenye hilo nalo lazima wachukuliwe hatua kali,"amesema Masaun.

Amefafanua wapo viongozi wa kisiasa ambao walikuwa wanatoa kauli za kuashiria uvunjifu wa amani ambao nao lazima wachunguzwe.

Amesema lengo la uchunguzi huo ni kupata taarifa sahihi ili asije kuoonekana hatua zimechukuliwa bila kufanyika uchunguzi, hivyo wameanza na uchunguzi ambao anaamini utakamilika kwa haraka.

Ameongeza uchunguzi huo utafanyika kwa weledi na umakini wa hali ya juu ili kuhakikisha haki inatendeka huku akieleza kwa sasa hawawezi kusema wamekamatwa watu wangapi kutokana na tukio hilo  ila uchunguzi ukikamilika watatoa taarifa kwa umma hatua zinazofuata.


RISASI ILIYOMUUA AQWILINA KUCHUNGUZWA

Masaun amesema kwenye uchunguzi huo utahusisha na risasi ambayo imetumika kumuua mwanafunzi huyo kwani ni mapema mno kutuhumu Jeshi la Polisi kulingana mazingira ya tukio hilo na kwamba hivyo ili kupata uhakika wake lazima risasi ichunguzwe kupata ukweli.

"Tunataka kujiridhisha na tukio hili na kwa mazingira hayo uchunguzi utafanyika hatua kwa hatua.Kama risasi imepigwa juu kwanini iende kupiga mwanafunzi aliyekuwa kwenye daladala.Kwa mazingira ya aina hii ndio maana tunasema acha uchunguzi ufanyike na ukweli utajulikana,"amesema.


Alipoulizwa uchunguzi utachukua muda gani?Masaun amejibu uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi huo pamoja na wale ambao wamejeruhiwa hautachukua muda mrefu kwani lazima ufanyike haraka na kwa weledi mkubwa.

"Weledi wa hali ya juu inahitajika kuchunguzi tukio hli ambalo limegusa hisia za wengi.Tunataka iwe fundisho kwa wengine kwani Serikali haiko tayari kuona raia wake wanauawa.Hatuko tayari kuona maisha ya raia  wa Tanzania yanatoweka,"amesema Masaun.


AZUNGUMZIA YA MTANDAONI, POLISI

Wakati huo huo, Naibu Waziri Masaun amesema kutokana na aina ya tukio la kifo cha mwanafunzi huyo wananchi wengi wamekuwa wakitoa maoni yao kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kufanya hivyo si kosa.

Amefafanua tu kwa wanaotoa maoni ni vema wakahakikisha hawavunji sheria za nchini huku akiomba ni vema kwa waliokuwa na taarifa sahihi badala ya kuzitoa mitandaoni watoa taarifa hivyo katika vyombo vya ulinzi ili zitumike kwenye kupata taarifa sahihi za tukio hilo.

"Milango kwetu iko wazi kwa wanaotoka kutoa taarifa kuhusu kifo cha mwanafunzi huyu.Pia wanaotoa maoni yao ni vema wakazingatia sheria.Serikali haiendeshwi kwa mashinikizo lakini ukweli kila mtu anayo nafasi ya kutoa maoni yake na kuelezea tukio hilo,"amesisitiza.


Kuhusu Jeshi la Polisi kutuhumiwa na mauji hayo , Masaun amesema si vema kulituhumu jeshi hilo kwani limekuwa likifanya kazi kubwa usiku na mchana kulinda usalama wa wananchi.

Amesema kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi kubwa ya kukabiliana na wahalifu nchini na kuelezea namna ambavyo limefanya kazi kubwa kudhibiti uhalifu maeneo mbalimbali yakiwamo ya Kibiti.

Amesema ni vema badala ya kutuhumi jeshi hilo ukaachwa uchunguzi ufanyike na baada ya hapo atakayebainika kuhusika hatua za kisheria zitachukua mkondo wake.

UCHUNGUZI MAUJI KADA CHADEMA

Kuhusu waliohusika na kifo cha aliyekuwa kada wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Masaun amesema uchunguzi unaendelea na sasa wanamhoji shahidi muhimu katika tukio hilo.

Ametoa ufafanuzi huo kutoka na taarifa za kwamba kifo cha kada huyo Jeshi la Polisi ndio linahusishwa kutokana na moja ya kauli ya viongozi wa ngazi za juu Chadema, ambapo Masaun amejibu uchunguzi utakamilika haraka na majibu yake yatashangaza wengi.

"Hili tukio la kifo cha kada wa Chadema nieleze tu uchunguzi unaendelea na kuna shahidi muhimu anaendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi.Hata hivyo kitakachotokea kitashangaza na kushtua wengi,"amesema Masaun.

ALICHOKISEMA RAIS MAGUFULI

Wakati hayo yakiendelea  Rais, Dk.John Magufuli kupitia akaunti yake ya twitter amesema hivi "Nimesikitishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwilini wa Chuo cha Usafirishaji(NIT).Natoa pole kwa familia .ndugu ,wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.

"Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili".

Share it:

habari

Post A Comment: