![]() |
Baadhi ya Nyaraka zikiwa zimechomwa Moto ndani ya Ofisi za Polisi Jamii mtaa wa Nyakabale Wilayani Geita. |
![]() |
Kiongozi wa polisi jamii katika mtaa wa Nyakabale Bw Nyeresi Charles,akielezea namna tukio lilivyoweza kutokea na wananchi kufikia hatua ya kuvamia ofisi zao. |
![]() |
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Geita ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Mwl Herman Kapufi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuona uharibifu kwenye kituo hicho. |
![]() |
Bomba la maji likiwa limekatwa na baadhi ya wananchi ambao walivamia kwenye kituo cha Polisi Jamii. |
Na,Joel Maduka,Geita.
Katika
hali isiyo ya kawaida Wananchi wa mtaa wa
Nyakabale na Manga kwenye Halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita wamekivamia
na kuharibu miundombinu ya kituo cha polisi jamii katika mtaa wa Nyakabale huku
jaribio la kukiteketeza kwa moto kituo
hicho likishindikana.
Tukio hilo limetokea
jana jumapili majira ya asubuhi ambapo inadaiwa kuwa kundi la watu zaidi ya 200
limevamia kituo hicho kwa madai ya kulipiza kisasi kutokana na mwenzao
aliyetambulika kwa jina la Zakaria Shaban (36) kudaiwa kupigwa na polisi
jamii ambao ni walinzi wa mgodi wa dhahabu wa Geita, GGM hadi kufa.
Hata hivyo kiongozi wa
polisi jamii katika mtaa wa Nyakabale Bw Nyeresi Charles amesema mtu huyo
ambaye inadaiwa ameuawa na Polisi jamii, inasadikika kuwa alipigiwa mgodini
Tarehe 7 mwezi huu na kwamba wanashangaa kuona wananchi wamekwenda kwenye ofisi
zao na kufanya uhalifu kwa kuharibu baadhi ya vitu huku wakijaribu kutaka
kuchoma Jengo ambalo limekuwa likitumika.
Mwenyekiti wa mtaa wa
Manga Bw Mtedi Lukanya
alisema hakuna mwenye uhakika wa
mtu kufa na kwamba kama alipigwa tarehe 7 mwezi huu hapo katikati kumetokea jambo
gani hadi kufanya uharibifu wa kuvamia ofisi siku ya Jumapili.
Mwenyekiti wa kamati ya
ulinzi na usalama ya wilaya ya Geita ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Mwl Herman
Kapufi amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akiwasisitiza wananchi kuachana na
desturi ya kujichukulia sheria mkononi na kwamba kama kuna tatizo ni bora
wavishirikishe vyombo vya dola na kama vinashindwa ni bora wakawasiliana naye moja
kwa moja.
Jeshi la polisi wilaya
ya Geita limefika katika mtaa huo na kuwakamata watu wanne wakiwemo wanawake
wawili na wanaume wawili na bado linaendelea na uchunguzi kuwabaini wengine
wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Post A Comment: