Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba
(katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la
kupiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa pombe aina ya viroba leo Jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na
Muungano Profesa Faustine Kamuzora na Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi hiyo
Richard Muyungi.
SERIKALI imepiga rasmi
marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki
maarufu kama viroba kuanzia tarehe 1 Machi 2017.
Hayo yamebainishwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano Januari Makamba
wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
“Dhamira ya Serikali
siyo kupiga marufuku vinywaji vya pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi
katika mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya,” alisema Makamba.
Aliongeza kuwa uamuzi
huo wakusitisha matumizi ya pombe hizo, Serikali itatumia Sheria ya Mazingira
ya mwaka 2004 ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa
maamuzi hayo.
Alizitaja taratibu
hizo kuwa ni pamoja na kutungwa kwa kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa
vifungashio vya plastiki kwa mujibu wa kifungu 230 (2) (F) CHA Sheria ya
mazingira ya 2004.
Aidha Waziri Makamba
ametoa wito kwa wazalishaji wa pombe kali wanaohitaji muda wa ziada wa kuhamia
katika teknolojia ya chupa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya kupewa kibali
cha kuendelea na uzalishaji huku wakihama kabla ya tarehe 28 Februari.
Makamba alisema kuwa
maombi hayo yaambatanishwe pamoja na ushahidi wa barua ikionyesha mwenendo wa
ulipaji wa kodi, nyaraka kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) kuhusu usalama
wa kinywaji, uthibitisho wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS),cheti cha tathmini
ya athari za mazingira, uthibitisho kuwa atatumia teknolojia ya kudhibiti
utengenezaji wa vifungashio bandia na uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni.
Katika hatua nyingine
Waziri Makamba amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini kuendesha operesheni kwa ajili
ya kudhibiti uingizwaji wa pombe kali zinazotoka nje na kuzuia matumizi ya
pombe haramu aina ya Gongo.
Utekelezaji wa uamuzi
huo unafuatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kusitisha matumizi ya
vifungashio vya plastiki ikiwemo pombe za viroba iliyotolewa bunge mwezi Mei
2016, Agosti na Desemba 2016 na kufuatiwa na agizo la Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa Majaliwa akiwa ziarani mkoani Manyara aliagiza kusitishwa kwa
utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zunazofungashwa kwenye vifungashio
vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi.
Na: Frank Shija -
MAELEZO
Post A Comment: