Rais wa Marekani Donald
Trump ametia sahihi amri mpya kuu ya uhamiaji ambayo itawazuia wahamiaji kutoka
nchi sita zenye waislamu wengi kuingia Marekani kwa muda wa siku 90.
Iraq imeondolewa kutoka kwa orodha ya nchi saba zilizoorodheshwa
awali. Watu wenye visa halali wataruhusiwa kuingia Marekani.
Hatua hiyo ambayo pia inajumuisha marufuku ya siku 120 kwa wakimzi
wote, itaaza kutekelezwa tarehe 16 Machi.
Amri ya awali ilifutilia mbali mpango mzima wa uhamiaji wa
Marekani, na kuwazuia raia kutoka nchi saba zenye waislamu wengi kuingia
Marekani.
Hatua hiyo ilizua fujo kwenye viwanja vya ndege wakati watu wenye
stakabadhi halali walizuiwa kuingia Marekani na pia kusababisha maandamano
makubwa.
Uongozi wa bwana Trump ulisema kuwa amri hiyo ni muhimu kuwalinda
Marekani kutokana na ugaidi.
Ilani ya siku 10 imetolewa ili kusaidia kuzuia fujo
zilizoshuhudiwa kwenye viwanja vya ndege tarehe 27 mwezi Januari wakati amri ya
kwanza ilipotangazwa.
Wasafiri waliokuwa na visa halali waliokua hewani wakati huo
walijipata wakizuiwa na maafisa wa mipaka walipowasili.