RAIS MAGUFULI-MARUFUKU MWANAFUNZI MJAMZITO KUENDELEA NA MASOMO

Share it:
unnamed



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete wakati wa hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Bagamoyo-Makofia-Msata yenye urefu wa kilomita 64, leo Wilayani Bagamoyo, Pwani. Mama Salma amekuwa mstari wa mbele kupinga mwanafunzi wa kike kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhwani Kikwete.
Picha na: Frank Shija – MAELEZO

Na. Frank Shija-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake haitoruhusu mwanafunzi aliyepata ujauzito kuendelea na masomo kama ambayo baadhi ya Asasi za Kiraia zinavyopiga kampeni kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.
Kauli hiyo imetolewa leo Wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani na Mhe. Rais alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Bagamoyo–Makofia-Msata, yenye urefu wa kilomita 64
“Nataka niwaambie ndani ya utawala wangu hakuna mwanafunzi mwenye mimba atakaye rudi shuleni, hayo ndiyo maisha aliyoyachagua, akalee huyo mtoto. Hata hivyo anaweza akaanza maisha mengine akaenda Veta, akajifunza kushona au kuchukua mkopo na kujiingiza katika kilimo cha kisasa,” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli aliongeza kuwa Serikali haiwezi kulipeleka taifa hili katika maadili ambayo hayapo katika jamii ya Kitanzania, hivyo kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na masomo ni kuharibu maadili ya Kitanzania.
Rais Magufuli amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wanapata elimu ndiyo maana alianzisha sera ya kutoa elimu bure, hivyo wanaopiga kelele kuwa watoto wa kike wanaopata ujauzito wapewe nafasi ya kuendelea na masomo wanataka kurudisha nyuma nidhamu ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli alimpongeza Mke wa Rais Mstaaafu wa Awamu ya Nne na Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete kwa juhudi zake za kupigania haki ya watoto wa kike kwa kupinga jambo hilo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea.
Aidha Rais Magufuli alisisitiza kuwa kamwe Serikali haiwezi kufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya Asasi za Kiraia na kuzishauri asasi hizo kuwa badala ya kuishawishi Serikali ichukue uamuzi wa kuwaruhusu watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo ni bora asasi hizo zikaanzisha shule zitakazotoa fursa hiyo.
Rais Magufuli amesema kuwa Sera ya Serikali ni kumsomesha mtoto bure na siyo kumfundisha azae na kwamba suala hilo halikubaliki katika Serikali yake na kusisitiza kuwa hakuna mwanafunzi mwenye mtoto atakaye ruhusiwa kuendelea masomo.
Hivi karibuni kumekuwa na mijadala bungeni na katika asasi za kiraia kuhamasisha Serikali iharakishe mchakato wa kuruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za msingi na sekondari mara baada ya kujifungua.
Share it:

habari

Post A Comment: