ALIYEKUWA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA GEITA AHUKUMIWA KWA MAKOSA YA RUSHWA

Share it:
















Image result for takukuru


 Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imemtia hatiani aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika kipindi cha mwaka 2008/2009 Bw. DAN LOITINGIDAKI MOLLEL kwa makosa mawili ya Matumizi Mabaya ya Madaraka kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya 2007 na kosa la Kuisababishia SerikaliHasara ya kiasi cha Tshs.4,450,000/= Kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwari la Kwanza, Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 iliyorejewa Mwaka 2002. Hukumu hiyo imetolewa leo tarehe 06/07/2017 na hakimu Mwandamizi wa Wilaya Mheshimiwa TIHO MRISHO.

Akiisoma hukumu hiyo mahakamani hapo ambapo upande wa jamhuri uliwakilishwa na Waendesha Mashitaka Bw. Kelvin Mrusuri, Augustino Mtaki na Bi. Felister Chamba, na Mshitakiwa alijiwakilisha mwenyewe, Mh. Tiho Mrisho alisema kwa kuwa Mshitakiwa amekiri kutenda makosa hayo akiwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita na kukubali maelezo ya awali ya makosa hayo mahakama imemtia hatiani kutokana na kukiri kwake makosa.

Baada ya kusomewa hukumu hiyo mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu  kabla ya kutolewa adhabu Mshitakiwa alisema Mahakama imwonee Huruma kwani umri wake ni miaka zaidi ya 70, amekuwa mtiifu kuhudhuria mahakamani katika kipindi chote, na kwamba ana wategemezi ambao ni wanafunzi wanaomtegemea, upande wa jamhuri ulisema hauna historia ya mshitakiwa kupatikana na hatia kwa makosa ya jinai.

Baada ya kusikiliza hoja za mshitakiwa na upande wa jamuhuri, Mahakama imemwachia kwa masharti ya kutotenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha miezi mitatu (3) pia Mshitakiwa anatakiwa kurejesha kiasi cha Tshs. 1,125,000/= ambayo ni sehemu ya Hasara aliyoisababishia Serikali. Kesi hii itaendelea tarehe 20/7/2017 kwa Washitakiwa wengine watatu (3) waliobakia katika kesi hii ya Uhujumu Uchumi Na. 7/2017.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita Bw. Thobias Ndaro anatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Geita waendelee kuiamini ofisi na kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa ili watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.
Imetolewa na:
Bw. Thobias Ndaro.
Mkuu wa TAKUKURU (M) GEITA
Share it:

habari

Post A Comment: