Kamati ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa leo imefanya ziara katika jengo la kitega uchumi la Rock City Mall ili kujionea utekelezaji wa mradi huo mkubwa Kanda ya Ziwa.
Na Binagi Media Group
Halmashauri za Jiji la Mwanza pamoja na Manispaa ya Ilemela mkoani
Mwanza, zimeendelea na mazungumzo ya namna ya kugawana mrahada wa mradi wa
kitega uchumi cha Rock City Mall, baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga ameyasema hayo leo
mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya utawala na serikali za mitaa iliyofanya
ziara ya kutembelea mradi huo pamoja na miradi ya barabaraba Jijini Mwanza.
Awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Jasson Rweikiza ilipongeza
ujenzi wa mradi huo, ingawa imesikitishwa ujenzi huo kutowekewa jiwe la msingi
wala jengo kuzinduliwa baada ya kukamilika huku wajumbe wengine wakihoji namna
mgawanyo wa mrahaba baina ya wabia wa mradi huo ulivyo.
Itakumbukwa kwamba ujenzi wa mradi huo ulianza mwezi Agosti mwaka
2012 baina ya wabia wawili ambao ni mfuko wa pensheni wa LAPF uliyochangia
bilioni 74.4 na halmashauri ya Jiji la Mwanza iliyotoa ardhi yenye thamani ya
shilingi bilioni 6.16 kabla ya mwaka 2013 Jiji hilo kugawanywa na kuzaliwa halmashauri
ya Manispaa ya Ilemela ulipo mradi huo na hivyo kufanya hadi mradi kukamilika
mwezi disemba 2015 wabia kuwa watatu.
Aidha gharama za mradi huo hadi kukamilika kwake ilipaswa kuwa
shilingi bilioni 74.4 lakini kutokana na ongezeko la gharama mbalimbali za
ujenzi, ujenzi huo uligharibu shilingi bilioni 80.56 huku makubaliano ya
mrahaba wa LAPF kuchukua asilimia 60 ya mapato ukiongezeka hadi asilimia 90.
Hatua hiyo ilipelekea mrahaba wa mapato wa asilimia 40 zilizokuwa
zikigawanywa kwa halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kushuka
hadi asilimia 10 hatua ambayo inazirejesha halmashauri hizo kwenye mazungumzo
ya namna ya kugawana mrahama huo kwani awali kila halmashauri ilikuwa ikichukua
asilimia 20.
Annette Shaoo ambaye ni Meneja wa kampuni ya Mwanza City
Commercial Complex Company Limited (MCCCCL) inayosimamia mradi huo, amesema mwezi
septemba mwaka huu makusanyo ya kodi yalifikia bilioni 2.9 kwa mwaka na kwamba
matarajio ni kufikia bilioni 4.2 kwa mwaka jengo likijaa wapangaji, ingawa kuna
changamoto kwa baadhi ya wapangaji kushindwa kulipa kodi ya pango na hatua
zimekuwa zikichukuliwa dhidi yao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa pensheni wa LAPF,
Mwanasheria wa mfuo huo Fidelis Mutakyamilwa amesema mapendekezo yaliyotolewa
na kamati hiyo ikiwemo kuboresha uendeshaji wa mradi huo yatafanyiwa kazi ili
kuvutia zaidi wawekezaji.
Katika kutamatisha ziara hiyo, pia kamati imekagua ujenzi wa
barabara ya Tilapia yenye urefu wa mita 600, Uzinza Rufiji mita 167, Isamilo
mita 800 ambapo barabara zote zimejengwa kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi
wa daraja la Msuka Kilimahewa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza (kushoto) akizungumza wakati kamati yake ilipotembelea mradi wa Rock City Mall. Kulia ni mwanasheria wa mfuko wa pensheni wa LAPF, Adelis Mutakyamilwa
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza (kulia) pamoja na Katibu wa kamati hiyo Chacha Nyakega (kushoto)
Mwanasheria wa mfuko wa pensheni wa LAPF, Adelis Mutakyamilwa akifuatilia mjadala wa kamati hiyo
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwanne Mchemba akizungumza wakati wa ziara hiyo
Mjumbe wa kamati hiyo, Venance Mwamoto akizungumza baada ya kutembelea mradi wa Rock City Mall
Mjumbe wa kamati hiyo, Zacharia Issaay akizungumza baada ya kutembelea mradi wa Rock City Mall
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga akizungumza kwenye majadiliano hayo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga (kushoto), Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza (katikati) pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye ziara hiyo
Post A Comment: